Benki ya Equity imesaini mkataba na kampuni ya umeme wa jua (solar energy) ya ZOLA Electric uliolenga kuwawezesha wateja wa benki hiyo kuunganishiwa umeme kwa mkopo.
Mkataba huo wa makubaliano, utawawezesha wateja wa benki ya Equity kuunganishiwa umeme majumbani bila dhamana huku wakilipa kidogo kidogo kwa kipindi cha miezi 18.
Mkurugenzi Mkuu wa Equity benki Robert Kiboti amesema “kupitia mkataba huu baina yetu na Zola, Benki itatoa mikopo kwa wateja wetu kununua vifaa hivyo ambapo kampuni ya Zola itawafikia na kuwawekea umeme mara moja baada ya benki kuwalipa”.
“Tunataka kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kwa wateja wetu, kwa kuwawezesha kupata umeme wa uhakika na gharama nafuu tutakuwa tumewasaidia katika kubadili maisha ya kutumia nishati isiyo salama,” amesema Kiboti.
Kiboti amesema “hata serikali imekuwa ikisisitiza juu ya nishati salama na ya uhakika”.
Amesema wateja wataweza kupata mkopo huo ambao unaanzia shilingi laki tatu na elfu thelathini na mbili (332,000/=) hadi shilingi milioni mbili (2,000,000/=).
Amefafanua kuwa wateja watalipa riba ya asilimia 16 mpaka 18.
Amesema zaidi ya familia million 8 nchini zinashindwa kupata umeme wa uhakika jambo lililowapelekea kushirikiana na Zola kuhakikisha wanapata nishati hiyo kwa gharama nafuu.
Ameongeza kuwa huduma hiyo imelenga kuwasaidia wateja kupata nishati hiyo mijini na vijijini.
“Hii inaenda sambamba na Malengo ya Maendeleo Endelevu lengo namba saba Nishati Mbadala kwa Gharama Nafuu,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Zola Electric Afrika Mashariki Johnson Kiwango amesema “watu wengi wanaogopa nishati mbadala kutokana na gharama, wananchi wanashindwa jinsi ya kulipa hivyo tumeona njia hii itawarahisishia”.
Amesema watanzania wengi hususani vijijini wanaishi maisha duni kutokana na kukosa nishati na kuhatarisha afya zao kwa kutumia nishati zisizo salama.
Kiwango amefafanua kuwa umeme huo utaanzia Watts 30 kwa nyumba ndogo ambao una uwezo wa kuwasha taa nne mpaka Watts 1000 kwa nyumba kubwa.
Equity benki ina matawi 14 yaliyopo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Moshi, Mbeya, Dodoma na Zanzibar ikiwa na mawakala zaidi ya 3600 na ATM 21.