Home BENKI Zanzibar yafungua dirisha la uwekezaji hati fungani inayofuata misingi dini ya Kiislamu

Zanzibar yafungua dirisha la uwekezaji hati fungani inayofuata misingi dini ya Kiislamu

0 comments 78 views

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefungua dirisha la uwekezaji katika hati fungani inayofuata misingi ya dini ya Kiislamu, Zanzibar Sukuk, ambayo inalenga kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo visiwani humo.

Akizungumza baada ya kikao na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya, kilichofanyika katika ofisi za Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu (BoT) Emmanuel Tutuba alieleza kuwa kuanzishwa kwa hati fungani ya Sukuk ni matokeo ya utafiti uliofanyika mwaka 2023.

Utafiti huo ulihusisha makundi yaliyo nje ya mfumo rasmi wa kifedha na kubaini kuwa baadhi ya watu, kutokana na imani zao za kidini, walikuwa wakishindwa kushiriki kwenye uwekezaji unaotoa riba.

“Kufuatia utafiti huu, tulifanya marekebisho kwenye Sheria ya Benki Kuu, Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha, pamoja na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ili kuwezesha utekelezaji wa masoko haya ya fedha kwa kuzingatia misingi ya Kiislamu,” alisema.

Aliongeza kuwa fursa hii ya uwekezaji inaruhusu wananchi wa ndani na nje ya nchi kushiriki kikamilifu, hivyo kuchochea matumizi ya huduma rasmi za kifedha.

“Ni uwekezaji halali kisheria unaowapa wananchi wote fursa ya kushiriki kulingana na imani zao, hivyo kusaidia miradi ya maendeleo ya serikali, kukuza uchumi, na pia kuwanufaisha wawekezaji,” alieleza.

Kwa upande wake Dkt. Saada Mkuya, alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kupata fedha kupitia hati fungani ya Sukuk kwa ajili ya kutekeleza miradi muhimu ya maendeleo.

“Miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali ya matibabu ya saratani ya Binguni, ujenzi wa kilomita 40 za barabara visiwani Unguja na Pemba, maboresho ya miundombinu ya umeme, na ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani,” alisema Dkt. Mkuya.

Alifafanua kuwa mwitikio kutoka kwa wananchi wa dini zote pamoja na taasisi mbalimbali umekuwa mkubwa, huku serikali ikilenga kukusanya shilingi trilioni 1.115. Katika awamu ya kwanza, lengo ni kukusanya shilingi bilioni 600.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!