Kampuni ya VHeines International wakishirikiana na kampuni ya KO wameandaa mkutano wao wa kwanza wa‘Dar Business Expo’ uliofanyika jijini Dar es Salaam leo hii.
Kusudi la kuandaa mkutano huo ni kushughulikia, kuunda uhamasishaji na mwelekeo madhubuti wa sera na mbinu zenye mkakati ili kuweza kujenga mahusiano yenye manufaa na mafanikio baina ya wafanyabiashara na taasisi za kifedha( binafsi na za serikali) hususani katika utoaji wa mikopo, ushauri, elimu nk.
Wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi mstaafu wa benki ya CRDB, Dokta Charles Kimei, ameeleza baadhi ya changamoto zinazosababisha wafanyabiashara wadogo na wakati kutokukua kibiashara ni pamoja na uoga wa wafanyabiashara wengi kukaribisha wawekezaji wengine katika biashara zao, masharti na vigezo vigumu wakati wa uombaji wa mikopo katika taasisi za fedha na wengi wao kutumia nguvu nyingi katika uboreshaji wa biadhaa na huduma kuliko suala la uwekezaji.
Dokta Kimei, amesema kuwa kutokana na utandawazi imekuwa ni changamoto kubwa kwa taasisi za kifedha kama benki kujenga ukaribu na wateja-wafanyabiashara hivyo kuna umuhimu kwa taasisi hizo kuendelea kuboresha huduma zao na kuziweka katika hali ya kisasa ili kuweza kujenga mahusiano ya karibu na wafanyabiashara.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mwananchi, Francis Nanai, ameeleza kuwa mbali na vijana kukosa ajira nakuamua kujiajiri. Inaelezwa kuwa 54% ya biashara ndogo na za kati (SMEs) zilizopo nchini zinamilikiwa na wanawake, huku asilimia 85 ya biashara hizo zikitoa ajira kwa watu mbalimbali na kuchangia 35% katika pato la taifa. Licha ya takwimu hizo Mkurugenzi huyo amesema kuwa si rahisi kwa biashara ndogo na za kati kufanya kazi zao vizuri ikiwa thamani ya fedha imeshuka, asilimia ya utoaji wa ajira nchini imeshuka ambao kwa upande wa ajira zinazotolewa na biashara ndogo na za kati asilimia imeshuka na kufika 30%..
Nanai, amewashauri wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini kuwekeza katika maeneo mengine ya huduma kama huduma za Tehama, intaneti, na nyingine nyingi zinazotokana na mabadiliko yanayotokea kila siku. Licha ya kueleza kuwa kuna umuhimu wa serikali kutengeneza sera zitakazowasaidia wafanyabiashara wadogo na wakati ,amewashauri wafanyabiashara nchini kujenga mazoea ya kusoma habari na machapisho mapya ambayo huchapishwa na serikali kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu uchumi wa nchi ili kuweza kuona fursa ambazo wanaweza kuzifanyia kazi.
Bwana Ivan Tarimo, Wanzilishi wa kampuni ya Bankable Tanzania, amewasisitiza wafanyabiashara nchini kuwa na rekodi maalum inayoelezea mapato, gharama za uendeshaji, na historia ya mikopo katika biashara ili kuweza kurahisisha hatua za mwanzo ikiwa wanataka kupata mikopo katika taasisi za kifedha hususani katika benki.
Pia, Mwanzilishi wa kampuni ya SSC Capital Tanzania, Salum Awadh, amesema kuwa kuna umuhimu kwa taasisi za kifedha kutengeneza huduma zinazoendana na mazingira yetu ili kuweza kujenga mahusiano mazuri baina ya wateja-wafanyabiashara na taasisi za kifedha. Na kusisitiza kuwa siku zote makundi hayawezi kufanya uvumbuzi bali watu binafsi wanaweza kuvumbua mambo mbalimbali na kutengeneza fursa zinazolipa.
Aidha, katika upande wa taasisi za kifedha mwakilishi wa masuala ya biashara kutoka katika benki ya NMB,Donatus Richard, amesema kuwa benki hiyo imekuwa ikifanya kila jitihada ili kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi nchini mbali na kuwa na matawi 230 Tanzania nzima. Baadhi ya maboresho ambayo wamefanya ni pamoja na kuwawezesha wateja wa benki hiyo kufanya miamala kwa kutumia simu janja kupitia programu waliyozindua hivi karibuni iitwayo ‘NMB mkononi’.
Baada ya mkutano huo wafanyabiashara waliohudhuria wameweza kufanya maonyesho ya bidhaa zao ili kuweza kujitangaza na kupata elimu baina yao.