Home BIASHARA Expedia Group ya Marekani kutangaza utalii wa Tanzania

Expedia Group ya Marekani kutangaza utalii wa Tanzania

0 comment 120 views

Kampuni kubwa ya biashara ya utalii duniani kupitia mtandao, Expedia Group, imeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Bodi ya Utalii (TTB), kutangaza na kuleta watalii wengi zaidi nchini.

Kauli hiyo inayounga mkono pia juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuitangaza Tanzania kimataifa, imetolewa Mei 8, 2023, na Mkurugenzi Mwandamizi wa Masoko ya Kimataifa wa kampuni hiyo, Andrew Van Der Feltz, alipokutana na kufanya mazungumzo kwenye makao makuu yao mjini Seattle nchini Marekani na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi.

Expedia ni kampuni inayotumia teknolojia za kisasa kutangaza na kuhudumia watu zaidi ya milioni 400 kwa mwezi duniani na ikiwa inatumia muunganiko wa zaidi ya tovuti 200 na ikifanya kazi na mashirika ya ndege na wabia wengine zaidi ya 509.

Expedia inashika nafasi ya pili duniani na wakati fulani namba moja Marekani kwa kuaminiwa na watalii katika sekta ya usafiri na utalii.

Awali, ujumbe wa Tanzania pia ulipata wasaa wa kusalimiana na Rais wa Expedia Group anayeshughulikia Biashara ya Kimataifa, Ariane Gorin, ambaye aliueleza aliwahi kutembelea Tanzania mwaka 2016 Tarangire, Serengeti na Ngorongoro Kreta kuwa ni nchi yenye vivutio vya kipekee na anatarajia kuitembelea tena.

Kwa upande wake Dkt. Abbasi aliyeambatana na Mtendaji Mkuu wa TTB, Damasi Mfugale, aliwahakikishia watendaji hao wa Expedia kuwa Tanzania kwa sasa imeamua kuja na mtazamo mpya katika kutangaza utalii.

“Tunaamini utaalamu wenu na uzoefu wenu katika masoko na biashara ya utalii kimtandao utasaidia kuongezea juhudi za Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya juhudi kubwa kupitia filamu ya “Tanzania; The Royal Tour” kuiweka Tanzania katika taswira pana zaidi kimataifa katika utalii na uwekezaji,” ameeleza Dkt. Abbasi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter