Jumla ya dola za Marekani 1.3 bilioni sawa na Sh trilioni 3 , zimetengwa kwa ajili ya hatua za awali za ujenzi wa jengo la gorofa 70 litakalojengwa katika kisiwa cha Chapwani Mjini Unguja, Zanzibar.
Jengo hilo litakuwa la kwanza Afrika Mashariki na kati kwa urefu ambapo litahusisha hoteli na maeneo mengine ya biashara.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kukamilika kwa makubaliano baina ya kampuni ya Kitanzania AICL Group na kampuni ya XCassia yenye utaalamu na uzoefu wa kusanifu na kuchora ramani za majengo marefu duniani kupitia uongozi wa Edinburg Crowland Management Ltd yenye ofisi zake katika majiji ya New York na Dubai.
Emmanuel Umoh ambae ni Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo wa AICL Group, amesema hoteli hiyo itakuwa na maeneo mengine ya kwa ajili ya biashara.
“Ujenzi wa hoteli hii utafanyika kwa awamu tofauti na unatarajia kukamilika baada ya miaka minne,” amesema
Mkurugenzi Mkuu na msanifu wa kampuni ya XCassia Jean-Paul Cassia amesema mradi huo ulitakiwa kuanza miaka mingi iliyopita lakini ulikwama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vikao, majadiliano, kukubali na kutokubaliana, tafiti za mazingira na kukosekana kwa mtu sahihi wa kuwekeza.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga amesema hatua hiyo ni Mapinduzi makubwa visiwani humo huko akionya watakaobainika kufanya urasimu wakati wa Utekelezaji mradi huo watachukuliwa hatua.
Jengo hilo litakaloitwa Zanzibar Domino Commercial Tower itajengwa umbali wa kilometa 15 kutoka Mji Mkongwe katika eneo la hekta 20 ikiwa na ukumbi mkubwa wa mikutano utakaobeba takribani watu 1,000.