Kampuni nyingi za kibiashara, wajasiriamali na wafanyabiashara kwa kawaida wamejaribu kufungua biashara zao na kuwekeza kwa kasi kubwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miundombinu bora ya utoaji huduma na bidhaa kwa kiwango cha juu, kuajiri wa wafanyakazi wengi na kuwapatia mishahara mizuri, kuimarisha ulinzi sambamba na wengine kutoa huduma ndani ya masaa 24.
Zipo sababu nyingi ambazo zinazofanya kampuni au wajasiriamali kupotea katika soko au kufilisika kabisa. Moja ya sababu hizo ni kutokujitangaza. Kuna faida mbalimbali za kujitangaza hasa kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na katika mabango japokuwa kuna changamoto zake pia.
Kampuni na wajasiriamali walio wengi waliowekeza katika kujitangaza wameweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na bidhaa zao au huduma zao kujulikana kwa umma na kwa eneo kubwa ndani ya muda mfupi. Hivyo ni vyema kabla ya kuanzisha biashara yako, ukawa na bajeti ili kuipa nafasi biashara yako ifahamike na watu wengi.
Kuna faida nyingi ambazo mjasiriamali na mfanyabiashara ataweza kupata endapo ataamua kuonyesha uthubutu wake katika kuitangaza biashara yake. Baadhi ya faida hizo ni pamoja na:
- Matangazo yanasidia kuongeza idadi ya wateja – Watu wanahitaji kusikia mjasiriamali/mfanyabiashara akija na kitu kipya kitakachomtofautisha na wafanyabiashara waliopo. Endapo umeanza biashara zamani lakini unahitaji kuitangaza onyesha kuwa kuna jambo jipya ambalo umeliboresha, umeongeza au utaenda kulifanya hivi karibuni ili kuongeza soko lako. Mara nyingi matangazo huwa yanaenda na ofa. Onyesha kuwa kuna faida watakayopata wakinunua bidhaa zako tofauti na wengine au watapata kitu wakitumia huduma yako.
- Matangazo yanaitengenezea biashara/kampuni yako mtazamo chanya kwa jamii – Wateja wengi na watumiaji wa huduma wanapenda kupata huduma ambayo iko wazi na inafahamika. Kuitangaza biashara yako kutaifanya jamii kuiamini biashara yako na kujua kuwa iko wazi na inafahamika na serikali na mamlaka nyingine hali itakayowajengea wateja uhakika wa kutumia bidhaa au huduma yako.
- Matangazo yanasaidia kuwavutia wateja – Mathalani umemtumia mtu maarufu kwenye tangazo lako na watu wengi wanampenda na kumwamini ni wazi kuwa watu wengi watavutiwa na biashara yako na kutamani kuinunua kwa sababu tu umemtumia mtu maarufu na hivyo kujihakikishia uwepo wa soko lako. Baadhi ya kampuni zimekuwa zikiwatumia wasanii wa muziki, vichekesho na mitindo pamoja na wachezaji ili kuongeza upana wa soko lao.
- Matangazo yanasaidia kuleta ushindani wa kibiashara – Mfano ni kampuni za mawasiliano. Limekuwa ni suala la kawaida kuwa kampuni moja inapokuja na tangazo la ofa sio muda mrefu kampuni nyingine nayo inakuja na ofa nyingine inayofanana nayo. Hii ni kuhakikisha kunakuwa na mvutano wa soko baina ya makampuni hayo ikiwa ni mojawapo ya njia zitakazosaidia kuongeza namba ya watumiaji wa mitandao yao (wateja).
- Matangazo yanasaidia kukuza kipato katika biashara yako – Jinsi unavyojitangaza ndivyo unavyokuza wigo wako na kuenea sehemu kubwa zaidi hivyo kuongeza wateja wako. Jambo la muhimu ni kuhakikisha sehemu ambayo matangazo yanafika huduma/bidhaa yako pia inapatikana vinginevyo itakuwa ni upotevu wa fedha.
- Matangazo yanasaidia kuwa na soko la uhakika – Ni dhahiri kuwa mtu anavyojitangaza ndivyo anavyojihakikishia uwepo wa soko. Kampuni au mfanyabiashara yoyote anashauriwa kuwa na matangazo mara kwa mara na kuonyesha uboreshaji na ukuaji wa huduma. Hii itaifanya jamii kuona uthubutu wako katika biashara na hivyo kuendelea kuiamini bidhaa yako.
Japokuwa kuna faida nyingi za kujitangaza, jambo hili lina changamoto zake pia. Kati ya changamoto hizo ni pamoja na:
- Matangazo yanahitaji pesa ya kutosha – Matangazo pia ni uwekezaji hivyo yana gharama kulipia hasa katika vyombo vya habari na Mabngo makubwa yanayopatikana katika miji mbalimbali nchini
- Kuwekeza sana kwenye matangazo kunaweza kupelekea kampuni kufilisika – Baadhi ya kampuni na wajasiriamali wengi wamejikuta biashara zao zikifa na kufilisika kutokana na kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika matangazo licha ya bidhaa zao kutofanya vizuri sokoni. Hali inayopelekea kushindwa kuwalipa waajiriwa na kuendesha huduma nyinginezo.
- Baadhi ya matangazo kufungiwa kwa kutozingatia maadili – Baahi ya kampuni zimekuwa zikifungiwa matangazo yao na serikali kutokana na kutofuata miiko au maadili ya kiafrika.