Kupata mshirika wa biashara bora inaweza kuwa si jambo gumu kwa wengi lakini jambo gumu ni kupata mshirika ambaye mtakwenda sawa (kwenye mtazamo na maamuzi ) na kuhakikisha malengo ya biashara yenu yanatimia.
Biashara nyingi za kushirikiana hushindikana sio kwa sababu washirika hawafanyi kazi kwa bidii, au washirika hawana uwezo wa kuifanya biashara husika, ila biashara aina hii hushindikana kwa sababu zifuatazo:
Kukabiliana
Kuogopa kukabiliana kuhusu masuala ya biashara huleta athari katika biashara taratibu na mwisho wa siku husababisha biashara isiendelee. Hivyo ni muhimu kwa wafanyabiashara kuelezana ukweli kwa ajili ya maslahi ya biashara. Ikiwa ukweli huo utapelekea maendeleo basi ni muhimu kuweka masuala binafsi pembeni. Kama washirika hamtakiwi kuogopana kwa namna yoyote ile.
Mawasiliano
Bila mawasiliano shughuli haziwezi kufanyika hivyo ni muhimu washirika katika biashara kuwasiliana kwa kuwa hii italeta urahisi kwenye kutatua matatizo ya kampuni kwa pamoja pia kwa kuwasiliana kila wakati kutaleta maelewano kuhusu biashara na namna ya kufanya biashara ikue zaidi.
Wajibu
Washirika wanatakiwa kupeana majukumu tofauti ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama inavyotakiwa. Mara nyingi washirika wa biashara huwa wanakuwa wametofautiana ujuzi na hata ikitokea wana ujuzi sawa lazima kuna vitu ambavyo vinawatofautisha. Ni muhimu kujua nani anaweza jambo gani zaidi kuliko jingine. Kwa mfano mmoja anaweza kuwa ni muongeaji na mwingine sio muongeaji hivyo muongeaji anaweza kujikita na masoko, au huduma kwa wateja.
Muda
Uvumilivu katika ushirika wa kibiashara ni muhimu. Na kuunda ushirika uliokamilika huchukua muda mrefu hivyo jua kuwa kufanya biashara ya ushirika kutakufanya ujue na ugundue mambo mengi kadili muda unavyokwenda. Pia muda utaleta mafunzo mengi ikiwa ni pamoja na kukabiliana na matatizo katika biashara, furaha ya faida na mwenendo wa mshirika mwenzako kipindi cha matatizo na furaha. Kujua vitu hurahisisha kazi kufanyika.
Malengo
Ni muhimu kutofautisha masuala ya kibiashara na masuala binafsi. Lakini ni muhimu kama washirika wa biashara wana malengo yanayoendana. Kazi itakuwa ngumu kufanya kama mshirika mmoja anafurahia kufanya kazi masaa mengi huku mshirika mwingine anapenda kufanya kazi masaa machache na kwenda kupumzika. Kuwa na malengo yanayoendana husaidi kuleta amani na utulivu katika biashara hivyo kabla hujashirikiana na mtu yeyote hakikisha wote mna malengo ya kimaisha yanayoendana hasa katika masuala ya kazi.
Urafiki
Sio kila mtu atakubaliana na hili lakini mshirika mwenzako katika biashara hatakiwi kuwa rafiki yako. Kwanini? Kwa sababu kwanza muda mwingi mnakuwa pamoja kwa sababu ya masuala ya kazi hivyo ni muhimu kuwa na maisha tofauti nje ya kazi/ofisi. Kushinda pamoja kila mahali kutasababisha mmoja wenu achoke. Hivyo kuwa na maisha tofauti nje ya kazi kutasaidia kila mmoja ajifunze mambo tofauti kutoka kwa marafiki zake na mambo hayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kusaidia biashara izidi kukua.
Utekelezaji
Ni rahisi sana kuongea kuliko kutenda. Ikiwa pande zote za ushirika zinapenda kuongea kuhusu mambo yanayoweza kufanyika kuhusu biashara lakini hakuna anayetekeleza mawazo hayo kwa vitendo basi biashara husika haiwezi kudumu muda mrefu. Hivyo ni muhimu katika ushirika kujikita zaidi na matendo kuliko maneno ili kuepusha kunyosheana vidole ikiwa mambo hayajaenda kama inavyotakiwa.
Hisia
Ili ushirika ufanye kazi ni muhimu kufanya mambo yanayohusu biashara kwa ushahidi kuliko kwa hisia. Kwa mfano kama fedha hazionekani badala ya kutumia hisia zako kuhisi kuwa mshirika mwenzako atakuwa amechukua na kwa namna moja au nyingine kumjulisha kuwa yeye ndio sababu fedha hizo hazipatikani, ni vyema kuchukua njia sahihi ya ushahidi kwa kufanya mahesabu na kuangalia matumizi yalivyokwenda ili kujua fedha hizo zimepoteaje. Kamwe hisia haziwezi kukamilisha malengo ya biashara au kampuni zaidi yataleta tu shida katika kufanya maamuzi na kukabiliana na mambo katika biashara.
Ni muhimu kuzingatia mambo haya ili kwenda sawa na mshirika/washirika wako katika biashara na kuhakikisha kuwa maendeleo yanakuwepo. Sio rahisi kujenga ushirika bora na wa kudumu katika biashara lakini muda na uvumilivu ni baadhi ya mambo ambayo yamewasaidia baadhi ya washirika kupata mafanikio makubwa.