Mahitaji ya nyama katika soko la nje ni makubwa kuliko uwezo wa uzalishaji hapa nchi.
Taarifa ya Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania, Tanzania Meat Board (TMB) Dkt. Daniel Mushi inasema masoko mengi ya nyama ya ngombe, mbuzi na kondoo yapo katika nchi za Mashariki ya Kati.
Ametaja masoko ambayo Tanzania inayo kwa sasa kuwa ni Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Kuwait, Oman, Comoro, Hong Kong,
Jordan na Saudi Arabia.
“Kwa mwaka jana tumeuza tani 10,415 yenye thamani ya milioni 42 za kimarekani na kwa robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha 2022/23 tumeuza tani 3,256.60 za nyama nje ya nchi zenye thamani ya Dola za marekani milioni 13,” amebainisha Dkt Mushi.
Ameeleza kuwa lengo ni kuuza tani 16,000 ifikapo 2026.
Amesema Tanzania inatakiwa ianze kushindana katika soko la nje ili iweze kunufaika na rasilimali hiyo.
“Kwa sasa kuku tunauza kiasi kidogo sana na tunapeleka Zanzibar pekee, hii ni kwasababu ufugaji wa kuku hauhitaji eneo kubwa,” amesema .
Amesema mpaka sasa Tanzania ina machinjio ya kisasa 22 na viwanda 19 vya kuchakata nyama ambapo machinjio tano ndio zimepewa ithibati ya kupeleka nyama nje ya nchi.
Ameeleza kuwa sheria inaeleza kuwa mtu yeyote haruhusiwi kufanya kazi au shughuli katika mnyonyoro wa tasnia ya nyama bila kusajiliwa na Bodi ya Nyama na kutambuliwa.
Dkt. Mushi amesema katika mwaka wa fedha 2022/23, Bodi imeidhinishiwa jumla ya shilingi 2,147,544,420 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.
Ametaja baadhi ya majukumu hayo kuwa ni pamoja na kuhakikisha wadau wote kwenye mnyororo wa thamani wa Nyama
wamesajiliwa na Bodi ya Nyama kwa mujibu wa sheria ya Tasnia ya nyama sura 421 ambapo jumla ya wadau 10,521 wamesajiliwa.
Kufanya ukaguzi wa kazi za wadau kwenye mnyororo wa thamani wa uzalishaji nyama ili kulinda afya za walaji kwa kuhakikisha wanapata nyama na bidhaa zake zenye ubora na usalama.
Kuhamasisha unenepeshaji wa mifugo ili kupata mifugo iliyo bora ambayo ni malighafi katika viwanda vya nyama, kuhamasisha wafugaji kubadilika kutoka ufugaji wa mazoea na kuanza kufuga kibiashara.
Nyingine ni kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo kwenye mnyororo wa uzalishaji nyama na bidhaa za nyama zikiwemo machinjio, viwanda vya kuchakata nyama, mifumo ya ubaridi na unenepeshaji pamoja na kuhamasisha ulaji nyama unaotakiwa ili watanzania wawe na afya bora.
“Tunalo jukumu na mkakati kama Bodi ya Nyama kuhamasisha Watanzania wale nyama, kuna watu wanasema nyama ni mbaya, lakini suala la nyama kuwa mbaya au nzuri ni suala la aina na kiasi cha nyama unayokula.
Kwa sasa Mtanzania mmoja anakula nyama takribani kilo 15 kwa mwaka lakini tunapaswa kula nyama angalau kilo 50 kwa mwaka,” ameeleza Dkt Mushi na kuongeza kuwa kwa wiki mtu mmoja anatakiwa kula kilo moja ya nyama.