Ni dhahiri kuwa matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii yameleta mafanikio makubwa katika biashara nyingi duniani, huku matumizi mabaya yamepelekea sifa mbaya kwa brandi nyingi hali ambayo imesababisha brandi hizo kupoteza asilimia kubwa ya wateja aidha kwa kujua au kutokujua.
Ili kutumia mitandao ya kijamii kwa usahihi na kwaajili ya mafanikio ya biashara yako, kuna mambo mengi ambayo yanatakiwa kubadilika. Hivyo basi yafuatayo ni makosa matano ambayo yanaweza kuharibu sifa ya brandi yako katika mitandao ya kijamii:
Kutokujibu malalamiko
Kila mfanyabiashara anatakiwa kujua kuwa si kila mteja atatoa mrejesho chanya baada ya kupata huduma au kununua bidhaa, hivyo mirejesho hasi ni kawaida katika kila biashara na ni muhimu zaidi kutokupuuzia mirejesho hiyo. Mfanyabiashara anapaswa kujua kuwa malalamiko katika biashara hasa yanayofanyika katika mitandao ya kijamii ni fursa ya kujua wapi wateja wanataka biashara iwe bora zaidi, na ni muhimu kujibu kitaalamu ili kuepuka kupoteza wateja wengi zaidi.
Hivyo, mfanyabiashara anatakiwa kujibu kwa ustadi na utaalamu malalamiko yanapotokea, kujifunza kutokana na malalamiko hayo, kuboresha bidhaa au huduma kutokana na malalamiko, ili kuepuka kupoteza wateja.
Matumizi ya Hashtag (#) zisizo na maaana
Sawa matumizi ya hashtag husababisha watu wengi kutazama maudhui yanayochapishwa katika akaunti ya biashara, lakini wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiweka hashtag zisizo na maana hali ambayo imekuwa ikisababisha maudhui hayo kutowafikia wateja husika.
Ili kuepuka hili, inashauriwa kuangalia akaunti nyingine ambazo zinafanya biashara inayoendana na yako kisha angalia hashtag wanazotumia na kujaribu kutumia hashtag hizo katika machapisho yako ( ziwe na maana). Kwa kufanya hivyo ujumbe unaochapa katika akaunti ya biashara utawafikia wale unaowalenga, brandi yako itakua na hata kupelekea kupata wateja wapya.
Kutokuwa na mawasiliano na wateja
Katika ulimwengu wa sasa wa biashara mawasiliano mazuri katika mitandao ya kijamii ni moja ya misingi ambayo hujenga wateja waaminifu katika brandi yoyote. Asilimia kubwa ya watu ambao ‘wanafollow’ akaunti yako ya biashara huvutiwa zaidi na brandi ikiwa kuna mawasiliano mazuri na ya binafsi na brandi hizo na wengi ‘hunfollow’ akaunti za biashara mara baada kutokujibiwa maoni, na waswali.
Hivyo kama ambavyo unawasiliana vizuri na wateja pindi wanapokuwa wamefika katika eneo lako la biashara unatakiwa kufanya hivyo hivyo katika mitandao ya kijamii kwani akaunti yako ya biashara ni uso wa biashara yako katika mitandao hivyo kwa ujumla unatakiwa kuhakikisha akaunti yako inavutia ili kuweza kujipatia wateja wapya na kuendelea kuwa na wateja wa zamani waaminifu huku ukijenga heshima katika brandi yako.
Kuwa na mitandao mingi kwa wakati mmoja
Badala ya kutumia mitandao mingi kwa wakati mmoja, kwamfano kuwa na akaunti facebook, instagram, twitter, pinterest nk unashauriwa kuzingatia mitandao miwili au mmoja kwaajili ya biashara kwasababu lengo ni kuhakikisha brandi yako inajulikana na wateja ambao wanahitaji bidhaa au huduma unayotoa.
Hivyo fanya utafiti ili kujua wateja wako wanatumia muda mwingi katika mitandao ipi ya kijamii kisha unda wasifu wako katika mitandao hiyo. Kwamfano kama wateja unaowalenga ni wafanyakazi, usipoteze muda kuunda akaunti pinterest, bali unda akaunti katika programu kama LinkedIn hapo utakuwa unayatendea haki maudhui unayochapisha katika akaunti yako.
‘Kupost’ sana
Kila kitu kikifanyika sana huleta madhara ambayo mara nyingi huwa si mazuri. Hivyo hata katika akaunti ya biashara inashauriwa kuwa na mipaka ya kuchapisha maudhui kuhusu biashara yako. hii itakusaidia kuleta umakini kwa watu wanaofuatilia akaunti yako, maudhui yakiwa mengi kwa wakati mmoja yanaweza kupelekea wafuatiliaji wako kupuuza machapisho hayo na hata kuacha kukufuatilia kabisa (Unfollow). Hivyo tenga muda sahihi wa kuchapisha maudhui kuhusu biashara yako, zingatia muda ambao wateja wengi wanakuwa wanatumia mtandao wa kijamii husika ili kuweza kupata washiriki wengi (traffic).
Aidha, unatakiwa kujiuliza, je wewe ungekuwa mfuatiliaji katika mitandao ya kijamii, ungefuatilia akaunti inayochapisha maudhui unayochapisha na hata kuwa mteja muaminifu? Ukipata jibu basi itakuwa rahisi kuona mambo yapi unatakiwa kuboresha au kuacha. Mbali na hayo, elimu haina mwisho hivyo hakikisha unajifunza kila baada ya muda kuhusu mitandao ya kijamii ili kuweza kutumia mbinu mpya kuwafikia wateja zaidi na kujenga brandi ya kuaminika na yenye heshima.