Dar es Salaam. Takribani watu 12 wamefariki dunia kwa mafuriko kutokana na mvua kubwa iliyonyesha October 13 jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Aboubakar Kunenge amesema kati ya vifo 12, vifo nane vimetokea Ilala na vinne Kinondoni.
Amesema waliopoteaza maisha Ilala ni wanaume sita na wanawake wawili huku Kinondoni wakiwa ni wanaume pekee.
“Vikosi vyetu vya kushughulikia maafa pamoja na wananchi na vikosi binafsi viliweza kuokoa wananchi 87 ambao walikuwa kwenye maeneo hatarishi zaidi,” amesema Kunenge.
Kunenge amesema “Jiji letu lilipata mvua kubwa October 13 na kuleta athari ikiwemo vifo 12, nyumba 800 zimeingiliwa na maji, na nyumba 107 zimezolewa na maji wananchi 480 wamekosa mahali pa kukaa,”.
Ametaja maeneo yalioathirika zaidi kuwa ni pamoja na Kisutu, Chakula Bora, Tupendane Manzese, Barafu, Kisiwani, Basihaya na jangwani.
“Ujumla Jiji lote lilipata athari mbalimbali kutokana na mafuriko, yameleta athari mbalimbali katika miundombinu ikiwemo barabara, umeme na madaraja” amesema mkuu wa mkoa.
Kunenge ametoa pole kwa familia zote zilizopoteza ndugu zao pamoja na wote waliopatwa na mafuriko.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) zinaonyesha kuwa kuna uwezekano wa mvua kubwa kunyesha Oktoba 15 hadi 16.
Kunenge amewataka wananchi kuchukuwa tahadhari kwa kuhakikisha wanafuatilia taarifa zinazotolewa na TMA ili kujikinga na athari za Mafuriko.
Mvua hiyo iliyonyesha kwa siku nzima pia ilisababisha madhara mengine mbalimbali ikiwemo biashara kusimama kutokana na mafuriko, ukosefu wa usafiri pamoja na foleni kubwa barabarani.