Home BIASHARA Maeneo yaliyotengwa rasmi yanawashinda nini wamachinga?

Maeneo yaliyotengwa rasmi yanawashinda nini wamachinga?

0 comment 123 views

Kadri siku zinavyozidi kwenda, ndio kunakuwepo na ongezeko kubwa la wafanyabiashara hapa nchini hasa katika miji mikubwa ya biashara kama vile Dar es salaam. Ongezeko hili mbali na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa zenye uhitaji mkubwa sokoni pia limepelekea wafanyabiashara wengi kufanya biashara zao kiholela maeneo mbalimbali ya miji. Hata baada ya serikali kupitia mamlaka husika kufanya jitihada za kutenga maeneo mbalimbali maalum kwa biashara ndogondogo watu wengi wameendelea kukwepa sehemu hizo na kuamua kufanya biashara zao katika maeneo wanayopendelea wao.

Unaweza kujiuliza kwanini wafanyabiashara hawa wanafikia maamuzi haya? Maeneo waliotengewa hayawatoshi? Kwanini wanauza katika maeneo ambayo sio rasmi? Serikali inachukua hatua gani kisheria dhidi yao? Vipi kuhusu usalama wa wateja na mali zao?

Huenda ushindani uliopo sokoni unawakimbiza katika maeneo rasmi ya biashara. Ni kweli kuwa ni vigumu kumvutia mteja kama watu kumi mnafanya biashara moja. Labda ni sababu mojawapo inayowakimbiza wafanyabiashara hawa na kuwasukuma kwenda maeneo ambayo wanaweza kumudu ushindani. Lakini kufanya hivi kunatatua tatizo? Watahama mara ngapi? Na huko wanapohamia hakuna ushindani? Idadi ya wateja inaridhisha? Kwanini wasiweke nguvu zaidi kuboresha huduma zinazotolewa ili kuwa tofauti na wapinzani wao na kujiweka katika nafasi nzuri zaidi?

Mbali na hivyo, wateja wengi huwa tunaamini kuwa, wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika maeneo rasmi yaliyotengwa huuza bidhaa zao kwa bei ya juu kuliko wale ambao hufanya nje ya maeneo hayo. Hivyo ili kupunguza gharama wengi huishia kununua mahitaji yao nje ya maeneo hayo japokuwa inawezekana gharama ni ile ile. Wateja wengi huishia mitaani na ni asilimia ndogo tu ndio hufanya manunuzi yao katika maeneo rasmi. Mtazamo huu ukibadilika miongoni mwa wanajamii, huenda wafanyabiashara watapata motisha ya kuendesha biashara zao katika maeneo wanayopatiwa na serikali kwani watakuwa na uhakika wa wateja.

Vilevile, kodi pamoja na tozo mbalimbali zinazokuwepo katika maeneo haya kwa kiasi fulani nazo zimechangia wafanyabiashara kufanya shughuli zao nje ya sehemu hizi. Wafanyabiashara wengi ni wadogo hivyo wanashindwa kumudu gharama za pango kwani zinakuwa kubwa kwao hivyo wanaona ni bora wakafanye shughuli zao sehemu ambazo hazitowaumiza kifedha. Wengi wamekuwa wakilalamika kuwa mamlaka husika zimekuwa haziangalii hali ngumu ya maisha na zimekuwa zikiwatoza gharama kubwa hali ambayo imepelekea wengi kushindwa kukaa katika maeneo hayo.

Japokuwa kuna changamoto mbalimbali katika suala hili, yapo mazuri pia. Mfanyabiashara kuendesha shughuli zake katika maeneo rasmi kunamuondolea wasiwasi kwani usalama unakuwepo sio tu kwake yeye bali kwa wateja pia. Biashara zinaendeshwa katika mazingira ya usafi hivyo inaondoa mazingira hatarishi ya magonjwa. Kufanya biashara kwenye maeneo haya pia inatoa fursa kwa wafanyabiashara kujifunza na kuwa wabunifu katika shughuli zao. Hivyo mamlaka husika zinapaswa kuendelea kuwahamasisha wafanyabiashara kutumia maeneo haya kwani yamejengwa hususani kwa ajili yao.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter