Home BIASHARA Njia Kuu 5 za kukuza biashara

Njia Kuu 5 za kukuza biashara

0 comment 122 views

Suala la ukosefu wa ajira si kwa Afrika Mashariki tu bali ni suala ambalo limeikumba dunia nzima hali inayopelekea walio wengi hasa vijana kutafuta kila njia mbadala ili kupiga vita umaskini. Watu wengi wamekuwa wakiikimbilia ni Biashara na Ujasiriamali. Ni kweli kuwa biashara ni nzuri na inalipa, lakini shida ambayo imekuwa ikijitokeza ni kwamba  walio wengi kutojua njia na misingi mizuri inayoweza kuwafanya wakafanikiwa katika biashara zao

Hivyo ni dhahiri kuwa pamoja na biashara kuonekana kuwa kimbilio la wengi sio wote wanaoingia kwenye biashara wanafanikiwa. Tafiti zinaonesha kwamba asilimia tisini ya biashara zinazoanzishwa zinakufa mwaka mmoja baada ya kuanzishwa. Na hata hizo zinazovuka mwaka mmoja asilimia tisini hufa baada ya miaka mitano. Hivyo kama mwaka huu zimeanzishwa biashara mia moja basi miaka mitano ijayo ni biashara moja tu itakayokuwa bado inadumu.

Kwanini biashara nyingi hazidumu?

Biashara nyingi zinakufa kutokana na ukosefu wa elimu muhimu kuhusiana na biashara na ujasiriamali. Lakini pia kutokuwa na nia ya dhati katika kufanya biashara pamoja na kuiga kile wanachofanya wengine kwa kudhani waweza kufanikiwa kama wao walivyofanikiwa.

Biashara ni rahisi sana kufanya ila ni ngumu kuendesha na kuikuza mpaka iweze kukupa faida kubwa sana. Ili uweze kuendesha na kukuza biashara itakayokupa faida kubwa ni muhimu kuchukua muda na kujifunza vitu vya muhimu vinavyohusiana na biashara.

Leo tutajifunza misingi mitano muhimu ya biashara ambayo kila biashara inatakiwa kuizingatia. Wewe kama mjasiriamali una jukumu la kujifunza na kufuata misingi hii ili uweze kufikia malengo yako kwenye ujasiriamali na biashara.

Njia kuu tano zitakazofanya biashara yako ifanikiwe:

Ili biashara yoyote iweze kudumu na kukua inahitaji kufuata misingi ifuatayo.

-Kutengeneza thamani.

Ili biashara iweze kukua na kutengeneza faida ni lazima itengeneze bidhaa au huduma ambayo ni ya thamani kwa wateja. Ni lazima utoe bidhaa au huduma ambayo watu wanaihitaji sana ili kuboresha maisha yao. Kama hujaanza biashara fikiria ni kitu gani cha thamani ambacho watu wanakihitaji ila wanakikosa, katika mazingira uliyopo. Haijalishi ni kikubwa au kidogo kiasi gani ila ili mradi unajua kinahitajika kwa kiasi kikubwa anza taratibu kisha endelea kujifunza nini cha kuongeza na nini cha kupunguza kwa kadri ya mahitaji ya watu wa eneo hilo. Hii ni njia sahihi kabisa inayoweza kuifanya biashara yako ndogo kuwa kubwa zaidi.

-Soko.

Kuwa na kitu chenye thamani pekee bado haikutoshi kutengeneza biashara kubwa, ni lazima kuwe na soko linalohitaji bidhaa au huduma hiyo. Hata kama soko lipo bado sio rahisi kwa kila mtu kujua kwamba unatoa huduma muhimu. Hivyo ni muhimu kutafuta soko la biashara yako kwa njia mbalimbali zikiwemo matangazo. Inakubidi uhakikishe watu wanajua uwepo wa biashara yako na utengeneze uteja ili watu waje kupata thamani unayotoa. Kukosa soko la uhakika ni chanzo cha kufa kwa biashara nyingi.

-Kuuza.

Ili biashara ikue ni lazima uweze kuuza thamani uliyotengeneza. Ni muhimu uweze kuwashawishi watu wanunue bidhaa au huduma unayotoa. Kuuza ndio moyo wa biashara ambapo kama usipokuwa makini ni rahisi kwa biashara kufa.

-Kufikisha thamani.

Ulinganisho wa fedha na huduma ni muhimu. Kama umewaahidi wateja wako kuboresha huduma au kutoa huduma nzuri basi fanya hivyo kwani endapo watagundua kuwa bidhaa au huduma unayotoa ni ndogo ukilinganisha na pesa wanayonunulia basi ni dhahiri biashara yako haitoendelea tena. Ikiwezekana waoneshe wateja wako kuwa umedhamiria kuwapa huduma nzuri na bora kwa kuwaonesha ukarimu wako pindi wanaponunua bidhaa au huduma.

-Fedha.

Fedha unayoifanyia biashara ina heshima yake. Jaribu kuitenga fedha unayoipata dhidi ya matumizi yako ya kawaida. Kitu kinachowagharimu watu wengi ni kutojua kuwa fedha ya biashara inatakiwa kujitenga kabisa na matumizi mengine ya kawaida. Kwa mfano walio wengi wamekuwa wakichukua fedha za biashara/mtaji kukidhi mahitaji ya familia. Hapo biashara haiwezi kudumu hata siku moja.

Hiyo ni misingi mitano katika kukuza biashara lakini pia haimaanishi kuwa kwa kuijua misingi hiyo ndio njia pekee inayoweza kukufanya ukafanikiwa au biashara yako ikukua zaidi, hapana hebu tuendelee kidogo Kuna sehemu waweza kwenda mfano mgahawa kujipatia chakula chako cha mchana lakini ukakuta bado hakijaandaliwa ndo kwanza wanapika, ukiangalia upande wa pili wa mgahawa upo mgahawa mwingine na vyakula vimepikwa lakini hakuna watu bali asilimia kubwa ya watu wamejazana hapo kwenye mghahawa uliopo wewe wakisubiria chakula.

Jiulize kwanini hawajaenda upande wa pili kujipatia huduma hiyo inayotolewa sawa na hiyo ya hapo ulipo? Kuna vitu unatakiwa kuviongeza ambavyo kwa mwonekano ni vidogo lakini hivyo ndivyo vyaweza kuineemesha biashara yako na ikaonekana ya thamani zaidi

Waonyeshe watu kuwa huduma yako iko bora kuliko wengine wanaokuzunguka hii inaweza kufanyika kwa;

  1. Kutoa ofa kwa wateja wako. Itasaidia kuwapa moyo na kujiona ni sehemu ya familia ya biashara yako.
  2. Ukarimu- Waonyeshe kuwa unawajali watu wa rika zote pasipo kujali dini, ukabila, rangi na ulemavu.
  3. Omba radhi pale unapohisi huduma au bidhaa ulizotoa zina dosari au hazijamridhisha mteja. Inatokea mara kadhaa mtoa huduma au bidhaa kumfokea mteja wake jambo ambalo halitakiwi. Muelekeze endapo amekosea sehemu siku nyingine atajirekebisha.
  4.  Epuka ubaguzi. Hapa kuna ubaguzi wa aina mbali mbali kama vile rangi, tabaka, ulemavu, ukabila n.k. Hii itasaidia kuinua thamani ya huduma unayotoa katika biashara yako. Amekuja mzee au mtu mlemavu, onyesha kuwa unawajali kwa kuanza kuwapa huduma wao kwani hata serikali mbalimbali duniani zimekuwa zikiwapa kipaumbele watu hawa.
  5. Nidhamu ya Muda. Kama ofisi yako inatakiwa kufunguliwa saa moja kamili Asubuhi kwa ajili ya utoaji huduma basi hakikisha unafika mapema kabla ya huo muda na kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya wateja wako.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter