Tanzania imetajwa kuwa ni nchi yenye nusu ya simba wote Duniani.
Rais wa Jumuiya ya Uwindaji ya Kimataifa, (SCI), Sven Lindqueast ameitaja Tanzania kuwa na asilimia 50 ya simba katika mkutano wa 50 wa Mwaka wa Uwindaji wa Kitalii jijini Las Vegas, Marekani.
Bw. Sven Lindquest amesema kwa hatua hiyo anaipongeza Tanzania kwa juhudi kubwa za uhifadhi uliopelekea wingi wa wanyamapori hao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameeleza kuwa nusu ya simba wote wapo Tanzania kutokana na uimara wa serikali katika shughuli za uhifadhi
Amesema kuimarika kwa shughuli za uhifadhi hususani kwa wanyamapori walao nyasi ni moja ya sababu ya kuwa na Simba wengi kutokana na uhakika wa chakula cha kutosha.
Amefafanua kuwa Simba hula wanyamapori walao nyasi na wanyamapori hao wamekuwa wengi kutokana na uwepo wa nyasi za kutosha na usimamizi bora wa maeneo ya Hifadhi
” Kubadilishwa mfumo kutoka wa kiraia kwenda katika mfumo wa kijeshi kwa watumishi wote wanaosimamia maeneo ya Hifadhi ni moja ya sababu ya simba kuongezeka Tanzania” amesema Dkt. Ndumbaro
Ameongeza kuwa idadi hiyo ni kutokana na serikali kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini kwa kuitengea Wizara ya Maliasili na Utalii bajeti ya kutosha inayotumika katika kuendesha operesheni mbalimbali za kukabiliana na ujangili.
Amesema Serikali imeweza kufanikiwa kukomesha tatizo la ujangili kwa zaidi ya asilimia 90 huku akisisitiza kuwa inatarajia kumaliza kabisa tatizo la ujangili kufikia asilimia 100% ifikapo mwaka 2025.
” Uthubutu wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan wa kuwa bega kwa bega na Wizara imekuwa chachu kwa Tanzania kuzidi kuongoza kwa uhifadhi wa maliasili zetu”.
Soma: Watalii Hispania wavutiwa na Tanzania