Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikiendelea kuwasisitiza wafanyabiashara kote nchini kutumia mashine za kodi za kielektroniki. Wafanyabiashara wengine wamekuwa waelewa na kununua mashine hizo kama ilivyoagizwa na serikali huku wengine wakisema wanashindwa kufanya hivyo kutokana na gharama kubwa ya kununua mashine za EFD. Mashine hizi zina umuhimu mkubwa kwa wafanyabiashara, wananchi na hata serikali. Makala hii inalenga kumuelimisha mfanyabiashara kuhusu matumizi ya mashine hizi pamoja na umuhimu wake.
Kwa kutumia mashine za EFD, unapata uhakika zaidi kuwa kodi inayotakiwa kwenda moja kwa moja serikalini. Tofauti na kipindi cha nyuma, mashine hizi zinaondoa wasiwasi wowote kuhusiana na masuala ya kodi kwani kila kitu hufanyika kielektroniki hivyo mazingira hayaruhusu udanganyifu wa aina yoyote ile. Sio rahisi kwa kodi kupotea kwa namna yoyote ile endapo mashine hizi zikitumika.
Wafanyabiashara wakiendelea kutumia mashine za kielektroniki, serikali nayo itakusanya mapato kwa urahisi zaidi na kuwezesha miradi mbalimbali ya kimaendeleo kufanyika. Ili nchi iwe na maendeleo ni lazima serikali ikusanye mapato ya kutosha ambayo yatasaidia shughuli mbalimbali za kimaendeleo kufanyika. Hivyo wafanyabiashara wakifuata mfumo huu, serikali itakusanya zaidi na maendeleo nayo yataonekana zaidi katika nchi yetu.
Mbali na hayo, mashine za EFD zina uwezo wa kuweka kumbukumbu za kodi ambapo unahifadhi taarifa zako zote muhimu kwa takribani miaka mitano. Hii ni njia rahisi ya wafanyabiashara kuweka rekodi bila ya kuhofia upotevu wa aina yoyote kwani wafanyabiashara wengi wamekuwa wakitumia njia ambazo sio salama hivyo wakati mwingine kumbukumbu zao muhimu hupotea. Lakini kwa njia hii ya kielektroniki, unakuwa na uhakika wa usalama wa kumbukumbu zako zote kwa muda mrefu. Hiyo pia inasaidia kuona mwenendo wako wa biashara kwa ujumla.
Baada ya kueleza yote hayo, ni muhimu kwa wafanyabiashara na watanzania kufahamu kuwa ni jukumu letu sote kulipa kodi ili kuleta maendeleo katika taifa letu. Hakutakuwa na maendeleo kama wananchi hawatatimiza wajibu wao wa kulipa kodi. Hivyo basi ni muhimu kama wananchi wakashirikiana na serikali ili kuhakikisha kuwa tunapiga vita janga kubwa la umaskini. Wafanyabiashara wanatakiwa kuunga mkono agizo hilo la serikali na kuanza kutumia mashine hizi za EFD kama inavyotakiwa.