Serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli imeamua kununua korosho yenyewe moja kwa moja kutoka kwa wakulima badala ya kutegemea wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo ikulu jijini Dar es salaam na Rais Magufuli katika hafla ya kuwaapisha mawaziri na manaibu waziri walioteuliwa kuchukua nafasi zilizoachwa wazi kufuatia rais kuamua kufanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri kwa kuwaondoa waziri wa kilimo Charles Tizeba na waziri wa viwanda na biashara Charles mwijage na nafasi zao kuchukuliwa na Japhet Hasunga aliyekuwa naibu waziri wa maliasili na utaliii na Joseph Kakunda ambaye anachukua nafasi ya mwijage katika wizara ya viwanda,biashara na uwekezaji.
Akizungumza katika hafla hiyo,baada ya kupewa taarifa ya idadi ya wafanyabiashara wa ndani na nje walliojiandikisha kufuatia agizo la waziri mkuu Kassim Majaliwa kuhusu wanunuzi wa korosho,Rais alisema haina haja yakuendelea nao na serikali itanunua korosho hizo kwa bei ya shilingi 3300 kwa kilo.
“Nafunga mjadala serikali itanunua korosho zote yenyewe na itanunua kwa bei ya shilingi 3300 kwa kilo na magodauni yote yatalindwa na jeshi”.alisema mheshimiwa Rais magufuli.
Ikumbukwe hivi karibuni kulikua na mgogoro kati ya wakulima na wafanyabiashara juu ya bei ya kilo ya korosho hadi kufikia serikali kuingilia kati kwa kukutana na wafanyabishara kujadili na kufikia makubaliano ya bei ya kilo moja isiwe chini ya shilingi 3000 japo suala hilo lilikua gumu katika utekelezaji wake.