Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe amesema soko kubwa la mifugo linatarajiwa kufunguliwa mpakani mwa Tanzania na Kenya, eneo la Namanga ili kudhibiti tatizo la utoroshaji mifugo nje ya nchi. Mwaisumbe amesema hadi kufikia Mei 29 mwaka huu, taratibu zote za kuanza rasmi kwa soko hilo zitakuwa tayari zimekamilika. Pamoja na soko hilo, Mkuu huyo wa wilaya pia amesema kiwanda kikubwa cha nyama kinatarajiwa kufunguliwa ifikapo Oktoba mwaka huu.
“Hatua zote mbili hizo zitafanya biashara ya mifugo kuwa rahisi ambapo wafugaji watanufaika kwani tozo mbalimbali zitalipwa na mnunuzi wa mifugo au nyama iliyosindikwa kiwandani”. Amesema DC Mwaisumbe.
Aidha, Mwaisumbe amesema uwepo wa Kituo cha Forodha cha Pamoja cha Namanga (OSBP) umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza urasimu uliokuwa unarudisha nyuma wafugaji. Kituo hicho pamoja na kuondoa urasimu pia kimeongeza ukusanyaji mapato kutoka Sh. 300 milioni hadi Sh. 500 milioni kwa mwezi.
“Kituo hiki ni muhimu katika kuhudumia watu na kurahisisha ufanyikaji wa biashara mpakani”. Amesema Mwaisumbe.
Imeelezwa kuwa Wilaya ya Longido ni wilaya ya pili mkoani Arusha kwa wingi wa mifugo ikiwa chini ya Wilaya ya Ngorongoro yenye inayoshika nafasi ya kwanza kwa kuwa na ng’ombe 222,909, kondoo 322,295 na mbuzi 423,813.