Baada ya ujenzi wa kiwanda cha sukari cha Mbigiri kilichopo katika kijiji cha Mbigiri, Dakawa wilayani Kilosa mkoani Morogoro kusimama, wakulima wa kijiji hicho wameomba serikali kuwasaidia kutafuta soko la miwa kwani walikuwa wanategemea kuiuza katika kiwanda hicho.
Wakulima hao wameeleza kuwa, viongozi mbalimbali waliwahamasisha kuzalisha miwa kwa wingi kila walipokuwa wakienda kukagua ujenzi wa kiwanda hicho ambapo wengine walichukua mikopo ili kuweza kuongeza uzalishaji wa miwa na sasa hawajui watatoa wapi fedha za kulipa mikopo hiyo.
“Tulihamasishwa kulima miwa kabla ya ujenzi wa kiwanda kuanza na sasa tumepoteza nguvu na rasilimali zetu na bado tunadaiwa Sh. 2 Bilioni na benki ya Azania iliyotupa mtaji wa kufanya hii, ni hasara sana kwetu. Kampuni ya Mkulazi Holdings na viongozi wa mifuko na serikali walituhamasisha tulime miwa, tulilima na tulichimba visima hadi leo hatuoni wakija, miwa inakauka, visima vina maji hawajayapima, sasa tumebaki kama yatima na hatujui nini cha kufanya”. Wameeleza wakulima hao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mkulazi Holdings Dk. Heldaritha Msita amekiri kuwepo kwa matatizo ambayo wakulima wameyaelezea na kusema kuwa serikali ina mpango wa kununua mitambo kwa ajili ya kiwanda hicho.
Ujenzi wa kiwanda hicho ulianza mwaka 2016 na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kushirikiana na uliokuwa mfuko wa PPF chini ya kampuni ya Mkulazi. Kiwanda hicho kilikuwa kinategemewa kuzalisha sukari tani 50,000 kwa mwaka.