Home BIASHARA Tanzania kuanza majadiliano mradi gesi asilia (LNG)

Tanzania kuanza majadiliano mradi gesi asilia (LNG)

0 comment 143 views

Serikali ya Tanzania inatarajia kuanza majadiliano ya utekelezaji wa mradi wa kuchataka na kusindika Gesi Asilia (LNG).

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amesema hayo wakati wa kikao chake na Timu ya Serikali ya Majadiliano ya mradi wa LNG, na kampuni za Shell na Equinor, jijini Dodoma.

Waziri Kalemani amesema serikali inataka kuanza utekelezaji wa mradi huo haraka iwezekavyo mara tu baada ya majadiliano kukamilika baina ya Serikali na wawekezaji.

Ameeleza kuwa taratibu zote zilizohitajika kufanyika zimekamilika na Serikali ipo tayari kuanza kwa majadiliano hayo ili mradi husika uanze kutekelezwa kwani ni muhimu kwa watanzania.

Kalemani amebainisha kuwa lengo la majadiliano hayo ni kuhakikisha kuwa Serikali inapata faida pamoja na wananchi wake na pia makampuni yote ambayo yatawekeza kwenye mradi huo yanapata faida.

Amesema serikali imetoa muda wa miezi 6 kukamilisha majadiliano hayo, ili kuweza kuingia katika hatua ya pili ya utekelezaji.

Wakati wakisubiri majadiliano, Dk. Kalemani ameelekeza kuanza mara moja kwa kazi ambazo hazitahitaji majadiliano ikiwemo kuwapa wananchi ufahamu kuhusu mradi  ili utakapoanza  utekelezaji wawe tayari na uelewa.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, amesema serikali imetoa muda wa kutosha wa utekelezaji wa mradi huo na kuwataka wale wote ambao wapo kwenye timu hiyo kufanya kazi kwa juhudi ili jambo hilo likamilike kwa wakati.

Unni Fjaer, Meneja wa kampuni ya Equinor ameeleza wapo tayari kukaa pamoja na Serikali ili kuweza kulifanyia kazi suala hilo na kuahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter