Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk. Mzee Suleiman Mndewa amesema sekta ya utalii inachangia asilimia 25 ya pato la ndani na asilimia 80 ya fedha za kigeni, jambo ambalo wataalamu wanasisitiza limechochewa kwa kiasi kikubwa na matumizi bora ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).
“Kwa kuwa ni kisiwa, Zanzibar inahitaji mifumo mizuri ya mawasiliano ili kuwavutia watalii wengi zaidi. Ni jambo lisilopingika kwamba watalii wanahitaji sana kuwasiliana na ndugu zao kwa kipindi chote wanapokuwa hapa”. Amesema Mndewa
Mbali na utalii, Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa mbali na mchango mkubwa kwenye sekta ya utalii, Tehama pia inachukua nafasi kubwa kwenye sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo ya kilimo na uvuvi.
“Kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano kwenye kilimo, kwa mfano, unaweza kutengeneza mfumo ambao utakuambia muda muafaka wa kufanya jambo fulani la kuhudumia mazao kama muda wa kumwagilia”. Amedai Mndewa.
Katika uvuvi, mfumo huo unaweza kumuongoza mvuvi kujua ni sehemu gani kuna samaki wengi na wapi hasa anaweza kupata soko, hivyo kurahisishia kazi na kuifanya rahisi na yenye tija.