Mkaguzi wa Viuatilifu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Tanania (TPRI) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Mausa amesema maduka zaidi ya kumi wilayani Kyela yamefungwa na baadhi ya wafanyabiashara kukamatwa kufuatia ukiukwaji wa Sheria na taratibu za uuzaji wa viuatilifu hivyo.
Akizungumza wakati operesheni hiyo ikiendeshwa, Mkaguzi huyo ameweka wazi kuwa, wanaouza viuatilifu wanapaswa kuwa na kibali kutoka TPRI na vilevile mafunzo maalum ya namna ya kuviuza.
“Tumefanya operesheni ya kushtukiza hapa Kyela na tumekutana na mambo ya ajabu kweli, watu wanaamua kuuza viuatilifu bila kufuata Sheria, wanafanya wanavyotaka mpaka inafikia mtu anauzia sumu kwenye chumba cha kulala watoto, hili halikubaliki hivyo tumewakamata ili tuwachukulie hatua za kisheria”. Ameeleza Mausa.
Mbali na hayo, Mkaguzi huyo amesema kuwa, wamekamata viuatilifu ambavyo havijasaliwa na taasisi hiyo lakini vinauzwa madukani, jambo ambalo amesema pia ni kinyume na Sheria.
“Tumekamata viuatilifu vingine vimetengenezwa nje ya nchi na havijasajiliwa nchini na TPRI, hili pia ni kosa kisheria, viuatilifu hivyo tumevichukua kwa ajili ya kwenda kuviteketeza”. Amesema Mausa.