Kamishna Mkuu Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere, amewataka wafanyabiashara wote nchini ambao wanapitia na kukumbwa na changamoto za kodi kuwasiliana na ofisi zilizo karibu nao ili waweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Kamishna Kichere ameyasema hayo alipotembelea kiwanda cha DI & PC kinachojishughulisha na utengenezaji wa vinywaji kilichopo jijini Dodoma na kuongeza kuwa, TRA ipo tayari kusikiliza changamoto zozote za kodi kutoka kwa wafanyabiashara na itazifanyia kazi kwa kushirikiana na wafanyabiashara hao ili kuhakikisha kuwa serikali inapata mapato kwa wafanyabiashara hao kulipa kodi ndani ya muda muafaka.
“Wafanyabiashara wale wenye changamoto za kikodi waje tukae tuongee nao,na tuone namna ya kuzishughulikia changamoto zao lakini pia nao walipe kodi kwa wakati ili tusonge mbele” Amesema Kamishna Kichere.
Kwa upande wake, mmoja wa wakurugenzi wa kiwanda hicho Katherine Mwimbe, amesema ujio wa Kamishna Mkuu wa TRA katika kiwanda hicho umeleta faraja kwao kwa sababu wamepata fursa ya kuwasilisha kwake moja kwa moja changamoto za kodi walizokuwa nazo na Kamishna amewahakikishia kuzifanyia kazi haraka.