Katika harakati za kupiga vita umaskini, kundi kubwa la watu hasa vijana wamekuwa wakiwekeza katika ubunifu wao ili kuja na vitu tofauti ambavyo vitawaingizia kipato. Ikilinganishwa na miaka ya nyuma, vijana wengi zaidi wamekuwa wakijiingiza katika masuala ya ubunifu wa mavazi. Biashara hii imejipatia umaarufu mkubwa miaka ya hivi karibuni. Mojawapo ya sababu ya hilo ni wabunifu wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii hasa Instagram kutangaza kazi zao hivyo kuwafikia wateja wengi zaidi ndani na hata nje ya nchi.
Awali, fani hii ilionekana kuwafaa vijana wa jinsia ya kike tu japokuwa kuna wabunifu wa kiume ambao wamefanya vizuri na wamefanikiwa kama vile Mustafa Hassanali na Ally Rehmtullah. Lakini kadri miaka inavyozidi kwenda, dhana hiyo imepoteza nguvu na tumeweza kushuhudia vijana wa kiume wakijikita katika ubunifu na kazi zao kupokelewa vizuri. Mabadiliko haya yanaashiria kuwa haijalishi jinsia yako, kama una kipaji na malengo, unaweza kufika mbali.
Ubunifu wa mavazi umekuwa suluhisho hata kwa vijana ambao wamehitimu masomo yao. Wengi wameona badala ya kuhangaika na kupoteza muda kusaka ajira, ni bora wawekeza kile kidogo walichonacho katika biashara hii kwani mavazi ni mojawapo ya mahitaji ya msingi kwa kila binadamu hivyo soko la biashara hii ni ya uhakika. Kinachotakiwa katika hili ni kuangalia wale unaowalenga na kufanya huduma yako kuwa rafiki ili bidhaa zako zipate soko kwa urahisi.
Vilevile, mbunifu wa mavazi anapaswa kwenda na wakati. Anatakiwa kufahamu kinachoendelea katika ulimwengu wa mitindo ili asipitwe. Kazi hii inahitaji umakini wa hali ya juu kwani unatakiwa kusikiliza kile mteja anachohitaji na kuhakikisha kuwa anaridhika na huduma anayopatiwa. Biashara hii kadri siku zinavyokwenda inakumbwa na ushindani katika soko lakini kinachowatofautisha wabunifu hawa ni vipaji vyao, gharama za huduma wanayotoa na namna wanavyojitangaza ili kuwafikia watu wengi zaidi.
Mitandao ya kijamii ina mchango mkubwa katika maendeleo kama ikitumika vizuri. Wabunifu wachanga wamekuwa wakitangaza biashara zao kwa urahisi na hivyo imerahisisha wao kuwafikia watu zaidi. Mitandao ya kijamii pia imekuwa inatumika kama kioo cha kuangalia kile wengine wanafanya na kujifunza, kuomba ushauri, kupata maarifa ili kuboresha biashara husika na kufanya kitu ambacho kitavutia idadi kubwa ya watu.