Home BIASHARA Umuhimu wa vifungashio katika biashara

Umuhimu wa vifungashio katika biashara

0 comment 282 views

Muonekano wa bidhaa una mchango mkubwa katika kumshawishi mteja kununua au la. Muonekano wa bidhaa unaweza kumfanya mtu anunue au asinunue na wafanyabiashara wengi wamekosa wateja kutokana na muonekano. Inaelezwa kuwa 72% ya wateja hushawishika kununua kutokana na muonekano wa bidhaa hivyo ufungashaji unatakiwa kufanyiwa tathmini ili kuweza kupata mafanikio sokoni.

Mafunzo mbalimbali yamekuwa yakitolewa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuhusu ufungashaji bora wa bidhaa lakini kuna umuhimu mkubwa wa kila mfanyabiashara na mjasiriamali kupata mafunzo ya aina hii kila yanapoandaliwa ili kuweza kuvutia wateja ndani na nje ya nchi na kutimiza malengo yake.

Ili kutengeneza vifungashio bora, na vinavyoweza kuwahamasisha wateja ni muhimu kuzingatia yafuatayo:

Utofauti

Ili bidhaa iweze kumvutia mteja kuna umuhimu mkubwa wa kuwa tofauti na bidhaa nyingine, ule upekee wa muundo wa bidhaa ndio huvutia wengi. Ni muhimu kuwa na kitu ambacho kitakupa utambulisho wako mwenyewe sokoni kwani kwa kufanya hivyo, ni rahisi kwa wateja kutambua bidhaa sokoni kutokana na utofauti wake. Unapokuwa na vifungashio vya aina yake, unakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kukabiliana na washindani wako.

Utamaduni wa bidhaa

Unapotengeneza muundo wa bidhaa yako, usiifikirie kama bidhaa bali ifikirie katika muundo wa mtu. Vifungashio vya bidhaa yako vinatakiwa kufikisha ujumbe au kutoa utambulisho fulani kwa watu wa aina fulani mara tu watakapoiona bidhaa yako. Hii itawarahisishia wateja kutambua kuwa bidhaa husika imetengenezwa kwa ajili yao pindi tu wanapoingia sokoni.

Washindani wako

Ni muhimu kuangalia washindani wako na kujifunza kutoka kwao ili uweze kutengeneza vifungashio vinavyovutia zaidi na vitakavyosababisha bidhaa kufanya vizuri sokoni. Inaelezwa kuwa makampuni makubwa huwekeza fedha nyingi ili kuhakikisha kuwa vifungashio au muonekano wa bidhaa zao unawavutia wateja hivyo ni vizuri kwa mfanyabiashara kutenga bajeti kwa ajili ya vifungashio bora.

Mbali na hayo, ni muhimu kwa kila mfanyabiashara kujiweka katika upande wa mteja na kujiuliza, kama yeye angekuwa mteja angeweza kununua bidhaa hiyo? Jiweke katika nafasi ya wateja wako ili kuweza kuwapatia kitu chenye ubora wa hali ya juu siku zote.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter