Ikiwa unataka kuanzisha biashara mtandaoni kuwa na wazo sahihi la nini utafanya ni muhimu. Kila mtu huamini kuwa wazo lake la biashara ni zuri na litaleta mafanikio makubwa mbeleni. Lakini kutokuwa na mpango madhubuti, uvumilivu, ujasiri,na maono ni dhahili kuwa biashara husika haitoweza kufika mbali.
Pia kupitia mtandao wa intaneti, blogu, na mitandao ya kijamii watu wengi wameanzisha biashara na kufanikiwa na biashara hizo.Hivyo hivi hapa ni baadhi ya vidokezo ambavyo vinaweza kumsaidia mtu yeyote anayetaka kuanzisha biashara yenye mafanikio mtandaoni:
Uwekezaji wako wa mwanzo ukoje?
Biashara yeyote huhitaji uwekezaji katika upande wa muda na fedha ili kuweza kuanza vizuri. Hivyo jiulize ni kiasi gani cha fedha unaweza kutoa wakati wa kuanzisha biashara yako mtandaoni? Epuka kuanzisha biashara ambayo itakubidi utumie fedha zenye matumizi ya muhimu kama chakula, makazi nk. Kwani ikiwa wazo hilo la biashara halijazaa matunda changamoto ya ukosefu wa mahitaji ya muhimu itatokea. Hivyo hakikisha fedha unazotumia kugharamia wazo la biashara zinatokana na akiba ya ziada. Hivyo anza kidogo, wekeza fedha kiasi ili hata mambo yasipokwenda sawa hasara itakayotokea isiathiri sana mtiririko wako wa fedha.
Kuna aina gani ya msaada/mafunzo yanayopatikana?
Siku zote mafunzo husaidia wamiliki wapya wa biashara kujifunza jinsi ya kusimamia faida na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza. Pia huwasaidia wamiliki kuongeza ujuzi kwa ujumla. kuna mafunzo mbalimbali ambayo hutolewa kupitia intaneti kuhusu biashara mbalimbali zinazofanyika mitandaoni hivyo kama mfanyabiashara makini unatakiwa kujua kuwa Kujiandikisha kwenye madarasa au kutafuta msaada haimaanishi kuwa hauwezi kuendesha biashara yako kwani kila siku mabadiliko hutokea hivyo kwenda sawa na mabadiliko hayo kutarahisisha kujua bidhaa au huduma zinazowahamasisha wateja kila siku hivyo kuteka soko kwa urahisi.
Uko tayari kusubiria faida?
Mwisho wa siku lengo la kuanzisha biashara ni kujipatia fedha na kupitia mitandao mfanyabiashara anaweza kutengeneza fedha kwa bajeti ndogo kwani kuitia mitandao hakuna ulazima wa kuwa na eneo la kufanyia biashara. jambo la msingi ni kuhakikisha unajiwekea malengo yenye uhalisia. Ikiwa unataka kupata faida za haraka basi hauko tayari kufanya uwekezaji husika. ila ikiwa uko tayari kusubiri matunda kutokana na biashara yako basi wekeza na kuendelea kusubiri kupata faida mbeleni kwani mambo mazuri hayataki haraka, wape muda wateja wako kuzoea huduma na bidhaa unazouza.
Je unaiamini biashara yako?
Ikiwa umeanzisha biashara ya bidhaa je, unaamini katika bidhaa hiyo? Ungeiona bidhaa husika ungeweza kuinunua? Ikiwa wewe mwenyewe huamini bidhaa yako ni dhahili kuwa hata watu wengine pia watapata ugumu wa kuiamini bidhaa hiyo,hali itakayopelekea biashara husika kushindikana.
Hivyo hivyo, katika upande wa huduma je, unaamini katika huduma unayoitoa? Ungekua wewe ni mteja ungevutiwa na kufurahia huduma husika? je kupitia huduma husika unaweza kuwasaidia na kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi?
Aidha, ni muhimu kwa mfanyabiashara kukumbuka kila wakati kuwa malengo ya biashara ndio ufunguo wa maendeleo ya biashara hiyo, bidhaa au huduma inayoanzishwa inatakiwa kuwasaidia wateja kwa namna moja au nyingine, na siku zote ni muhimu kuamini katika biashara unayoifanya.