Kabla ya kuanzisha biashara, ni muhimu kufanya utafiti wa kina ili kujua ni wakina nani hasa unawalenga sokoni. Unapofanya hivyo, inakuwa rahisi zaidi kuandaa mkakati ambao utakuwezesha kuwafikia wateja wako kwa urahisi bila kutumia fedha nyingi kufanya matangazo na kutafuta wateja.
Ni mbinu gani unaweza kufanya kufanikisha hili? Una uhakika kuwa bidhaa au huduma unayotoa inawagusa wateja moja kwa moja? Haya ni maswali machache tu ambayo unatakiwa kujiuliza kabla ya kuwekeza katika biashara.
Hapo chini ni baadhi ya mambo ambayo unaweza kufanya ili kufahamu wateja wako sokoni.
Jihudumie mwenyewe kwanza: Asilimia kubwa ya wajasiriamali waliofanikiwa wametumia njia hii kutathmini wateja wao. Unapokuwa mteja wako mwenyewe, unakuwa na uhakika na nini hasa mteja anapata kutokana na bidhaa/huduma yako. Unapoanzisha biashara, usifikirie tu kuwa unatambulisha bidhaa sokoni, fikiria kwamba unatatua tatizo ambalo tayari lipo katika jamii inayokuzunguka.
Washirikishe marafiki: Kama unaweza kuuza bidhaa kwa marafiki na watu wako wa karibu, basi upo katika nafasi nzuri ya kufanikiwa sokoni. Mbali na hayo, marafiki zako wa karibu ni kundi ambalo linaweza kukushauri vizuri nah ii husaidia biashara kufanya maboresho mara kwa mara hivyo kuwapa wateja huduma/bidhaa iliyo bora kabisa.
Usijisahau: Baada ya biashara kukua na kufanya vizuri, ni rahisi sana kujisahau na kusahau ulipotoka. Hii haimaanishi kuwa hutakiwi kuboresha, kuimarisha na kutafuta mbinu nyingine mpya za kukuza biashara yako. Unaweza kufanya yote hayo, lakini inashauriwa kukumbuka mwanzo wako na kuendelea kutoa huduma ambayo wateja wako wa mwanzo wanaweza kuendelea kumudu kwani wana mchango mkubwa katika mafanikio ya biashara yako. Mfano mzuri wa hili ni Airbnb. Joe Gebbia na Brian Chesky, waanzilishi wa mtandao huu mkubwa duniani kwa sasa walianza kwa kupangisha magodoro na kutengeneza fedha kupitia nafasi ndogo ambayo walikuwa hawatumii. Japokuwa mtandao huu umekuwa na kufanyiwa maboresho makubwa, bado wanaruhusu watu kupangisha magodoro na vitanda katika makazi yao. Hii inaonyesha wanathamini walipotoka na bado wanaendelea kuwawezesha wengine wenye hali ya chini kutengeneza kipato cha ziada.
Kuna faida kubwa ya kujua nani hasa ni wateja wako. Aidha, biashara inakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kupata wateja na kufanikiwa ikiwa unafahamu soko lako tangu mwanzo. Japokuwa inaweza kuwa kazi ngumu kidogo kutambua wateja wako, hili ni suala ambalo linawezekana kwa asilimia 100. Ni muhimu kufanya utafiti wa kina katika hili kabla ya kuanzisha biashara.