Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Jeremiah Temu amesema licha ya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika mashariki kwa wingi wa mifugo ikilinganishwa na nchi nyingine katika ukanda huo, bado haijafikia kiwango cha mahitaji ya maziwa yanayotakiwa kuzalishwa kwa mwaka, ambacho ni lita 2.6 bilioni.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa maziwa Temu amedai kuwa kutopatikana kwa kiasi hicho kunairudisha nyuma sekta ya maziwa na kuongeza kwamba uzalishaji huo umekuwa mdogo ukilinganisha na uhitaji ambao kwa wastani ni lita 2.6 bilioni. Kwa mwaka 2016/17, Tanzania imeweza kuzalisha lita 2.1bilioni huku 2017/18 ikipanda hadi lita 2.4 bilioni.
“Kiwango kinachozalishwa sio chote kinachoenda kwa mlaji jambo linalosababisha sekta hii kurudi nyuma endapo vingejengwa vituo vya ukusanyaji ingesaidia kufikisha bidhaa hiyo sokoni” Ameeleza Temu.
Msajili huyo pia ameweza kufafanua kuwa hadi sasa vipo vituo 180 vinavyokusanya maziwa nchini huku kati ya hivyo, ikiwa ni asilimia 30 tu ndivyo vinavyofanya kazi.
“Nawasihi wadau na sekta hii kuwekeza katika ujengwaji wa vituo vya kukusanya maziwa kwa kushirikiana na vyama vya ushirika ambavyo vitahusika katika kuendesha vyama hivyo”.