Mtaji ni msingi wa ukuaji wa biashara yeyote, imekuwa ni kawaida kuona wajasiriamali au wafanyabiashara wapya wanafunga biashara zao kutokana na ukosefu wa fedha za uendeshaji wa biashara zao. Mbali na mikopo ambayo hutolewa katika mashirika ya fedha kwa wajasiriamali kuna njia mbalimbali ambazo wajasiriamali wapya wanaweza kupata mitaji na kuweza kutimiza malengo ya biashara zao, moja ya njia ya kupata mitaji ni kupitia ‘Angel Investors’.
Hivyo basi Angel investors ni nani? Hawa ni watu binafsi au katika makundi ambao huwekeza katika biashara ndogo ndogo ambazo zinaanza (startups). Mbali na mtaji, wawekezaji hawa hutoa utaalam wao kwa biashara husika ili ziweze kukua na kupanuka zaidi. Uwekezaji huu hufanyika katika kipindi maalum kulingana na makubalino kwa mfano miaka 5, 10 nk. Ili kuweza kupata kupata mtaji kutoka kwa wawekezaji wa namna hii inashauriwa kuhudhuria mikutano,hafla,semina mbalimbali zinazohusu masuala ya biashara na uwekezaji, ingawa unaweza kupata muwekezaji wa namna hii kupitia intaneti na hata katika vikundi.
Mpango wa biashara (business plan) ni moja ya mambo ya msingi ambayo yanaweza kumuhamasisha muwekezaji wa namna hii kuwekeza katika biashara mpya. Hivyo ikiwa umepewa fursa ya kuwasilisha mpango wa biashara yako hakikisha mpango huo unaeleza kila kitu kuhusu biashara yako kwa urahisi ili mtu ambaye hajui chochote juu ya biashara yako aweze kujifunza kila kitu kupitia maelezo yaliyopo katika mpango wa biashara na kuweza kufanya maamuzi sahihi.
Inaelezwa kuwa 50% ya wawekezaji wa namna hii huona urahisi wa kuwekeza katika biashara ikiwa wanaelewa ni nini hasa wanafadhili, fedha zao zinakwenda wapi hasa katika kampuni zinazoanza. Hivyo ni muhimu kufanya utafiti hasa kama unaanza kuhusu bidhaa au huduma unayotaka kuiuza, umewalenga wateja wa aina gani nk ili kuweza kumhakikishia muwekezaji wa namna hii kuwa kuna soko na kupitia uwezeshaji wake mbeleni kutakuwa na mafanikio baina ya pande zote mbili.
Timu yenye uzoefu, suala la usimamizi ni muhimu katika kila biashara. Hivyo wawekezaji wa namna hii huangalia usimamizi wa mwanzo katika biashara kabla ya kufanya maamuzi ya kutoa mtaji katika biashara husika. mbali na wazo la biashara, teknolojia zinazotumika kuendesha operesheni za biashara watu walio nyuma ya hayo yote ni muhimu pia. Ikiwa timu husika ina wafanyakazi wenye uadilifu, uwazi katika mikakati ya biashara na mbinu zitakazotumika, taaluma na nia itakuwa ni rahisi kwa biashara hiyo kupata mtaji kutoka kwa wawekezaji hawa.
Katika hali ya kawaida wawekezaji hutafuta fursa ambazo zitawanufaisha, hivyo kabla Angel Investor hajawekeza katika biashara yako ni dhahiri kuwa atataka kujua utabiri wako kuhusu marejesho ya ufadhili wake/wao. Je, ni kiasi gani wategemee kutengeneza ikilinganishwa na kiasi ambacho wanaweza kupoteza kwa kufanya uwekezaji katika biashara yako? kutokana na hilo ni muhimu kujua kuwa si kila muwekezaji anataka faida ya fedha, wengine hufarijika pindi wanapoweza kutatua changamoto kubwa duniani kupitia biashara wanazokuwa wanafadhili. Hivyo mfanyabiashara anaetaka kupata mtaji kupitia wawekezaji wa namna hii anatakiwa kuhakikisha biashara au huduma anayoanzisha inalenga kunufaisha jamii kwa namna moja au nyingine.
Wawekezaji wa namna hii mara nyingi huchukua faida zinazoanzia 20% hadi 50%. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa makubaliano yote yanaandikwa katika nyaraka, mwanasheria anapitia makubaliano hayo ili pande zote mbili ziwe katika upande salama.
Muda wa makubaliano ukiisha muwekezaji anaweza kuuza hisa zake kwa mfanyabiashara au kwa watu wengine au kuendelea kuwekeza kulingana na makubaliano ambayo hufanyika upya baina ya pande hizo mbili na hali ya ukuaji katika biashara hiyo.
Hivyo, licha ya kuwa uwekezaji wa namna hii ni wa hatari (risky) Angel Investor anaweza kupata fedha nyingi ikiwa ana uzoefu na tasnia husika. utafiti ni muhimu sana kwa muwekezaji na hata mfanyabiashara ili kuepukana na mkanganyiko wa aina yoyote mbeleni. Pia ni muhimu kwa pande zote mbili kusaini mikataba kabla ya kufikia hatua ya kutoa na kupokea mtaji.
Kwa Tanzania, TAIN (Tanzania Angel Investors Network) ndio mtandao wa kwanza ambao ulianzishwa mwaka 2018 kwaajili ya kuwaunganisha wafanyabiashara na wawekezaji wa mfumo huu.