Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka mahakama nchini kuharakisha kusikiliza kesi za kibiashara.
Rais Samia amesema hayo wakati akihutubia maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Februari 01, 2023.
Amesema ni vema mahakama ikatoa kipaumbele cha kuharakishwa usikilizwaji wa kesi za kibiashara katika masuala ya kisheria pindi inapotokea migogoro ili kuvutia mitaji na uwekezaji na kufungua fursa za biashara.
“Tunapovutia mitaji na uwekezaji nchini na kufungua fursa za kibiashara tunatambua kwamba uwekezaji huambatana na maswala ya kisheria na migogoro ya kibiashara. Ni vema mahakama zetu kutoa umuhimu kwa mashauri ya aina hiyo pia,” amesema Rais Samia.
Ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na wadau wa usuluhishi kubainisha maeneo yanayotakiwa kufanyiwa kazi ikiwemo kutunga sera ya usuluhishi.
Aidha, Rais Samia amesema ni wakati muafaka wa kujielekeza kufanya utatuzi kwa njia ya usuluhishi bila kufungwa na masharti ya kiufundi yanayokwamisha kutenda haki.
Ameitaka Wizara hiyo kushirikiana na wadau kutekeleza kikamilifu utoaji wa msaada wa kisheria kwa kuzingatia Ibara ya 107A ya Katiba inayowataka kutenda haki kwa wote bila kujali hali zao za kijamii au kiuchumi.
Vile vile, Rais Samia amesema mitazamo ya wadau wa Mahakama nchini haina budi kujielekeza kwenye kupunguza muda unaotumika kwenye mashauri ili wananchi watumie muda wao mwingi kwenye uzalishaji mali.
Amebainisha kuwa serikali inafanya jitihada kuimarisha upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi wasio na uwezo kupitia Mama Samia Legal Aid Campaign kwa kuwa kuna uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria nchini.
Kampeni hiyo tayari imewafikia wananchi 383,293 katika Mikoa 6 ya Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma, Simiyu na Singida ambapo imeweza kutatua migogoro takribani 511.