Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameeleza kuhusu mpango wa kuanzisha kitengo cha uwekezaji (One Stop Center) ili kurahisisha shughuli za uwekezaji na kuepuka changamoto zinazopelekea baadhi ya wawekezaji kukata tamaa. Makonda amesema hayo baada ya kutembelea ofisi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na kufanya mazungumzo kuhusu namna mbadala ya kuweka mazingira bora ya kibiashara ili kuondoa kero zinazowakabili wawekezaji na wafanyabiashara jijini Dar es salaam.
Makonda amedai kuwa kitengo hicho kitahusisha watendaji kutoka taasisi za Kituo cha Uwekezaji (TIC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Idara ya Uhamiaji na wadau mbalimbali wanaohusika na biashara.
“Naamini ushiriki wa TPSF katika ziara ya Rais Dk. John Magufuli jijini Dar es salaam hivi karibuni itakuwa fursa kubwa kwa sekta zote ikiwemo biashara, uchumi, afya, elimu, miundombinu na maji hivyo niwahimize watu wote kuitumia vizuri ziara hiyo ili kufikia ndoto ya Dar es salaam kuwa jiji la kibiashara”. Amefafanua Mkuu huyo wa mkoa.
Naye Mkurugenzi wa TPSF, Godfrey Simbeye amesema taasisi hiyo ipo tayari kufanya kazi na kutoa ushirikiano kwa Mkuu wa mkoa, katika harakati mbalimbali za kuboresha jiji la Dar es salaam.