Home BIASHARAUWEKEZAJI Kiwanda cha Twiga kuwekeza kiwanda cha saruji Tanga

Kiwanda cha Twiga kuwekeza kiwanda cha saruji Tanga

0 comment 110 views

Serikali imewahakikishia watanzania kuwa uwekezaji mpya wa zaidi ya dola za Marekani milioni 400 utakaofanywa na kiwanda cha saruji cha Twiga kwenye kiwanda cha saruji Tanga, utaongeza uzalishaji wa saruji, kukuza ajira na mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigilu Nchemba pamoja na Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji wamesema hayo walipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa kiwanda cha Tanga Cement, Jijini Dodoma.

Dkt. Kijaji amesema Kiwanda cha Saruji cha Tanga kupata mwekezaji mpya lilikuwa jambo lisilokwepeka kutokana kiwanda hicho kupata hasara kwenye mizania yake ya biashara kwa miaka mitano mfululizo na hivyo kuweka rehani zaidi za ajira za wafanyakazi 3,000 wa kiwanda hicho pamoja na mapato ya Serikali.

Amesema kuwa mtaji huo wa dola za Marekani milioni 400, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 930, utakifanya kiwanda hicho kuzalisha saruji kwa wingi itakayokidhi soko la ndani, Afrika Mashariki, na Eneo Huru la Biashara la Afrika kwa ujumla.

“Tunaamini kuwa Kiwanda cha Tanga Cement kitaongeza uzalishaji kwa kiwango chake cha mwanzo na kuendelea kutoa ajira za watanzania 3,000, pamoja na matarajio ya kiwanda hicho kuanza kulipa kodi Serikalini baada ya mwaka mmoja ujao” ameeleza Dkt. Kijaji

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema uamuzi wa Serikali wa kukinusuru kiwanda hicho umechukuliwa kwa umakini mkubwa na kuishauri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuharakisha uwekezaji huo ili ukamilike kama ilivyopangwa.

Amesema kiwanda hicho kina mchango mkubwa wa kukuza ajira, kutoa kodi Serikalini lakini kikubwa ni kuongezeka kwa uzalishaji wa saruji kunakotarajiwa ambako kutawafanya wananchi wapate saruji kwa bei nafuu ili kujenga makazi bora.

“Uzalishaji ufanyike ili wananchi wapate saruji ili wajenge nyumba bora, na watafanya hivyo bei ya saruji ikiwa chini, uzalishaji ukiwa mkubwa, tunauhakika wananchi watapata sementi kwa bei nafuu” ameeleza Dkt. Nchemba.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter