Na Grace Semfuko-MAELEZO
Sera nzuri za uwekezaji zinazotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, zimeanza kuzaa matunda ambapo Serikali ya Libya inaangalia uwezekano wa kuja kuwekeza katika sekta ya Nishati ya umeme.
Kaimu Balozi wa Libya hapa Nchini Saleh Kusa Arze, amesema tayari wameziona fursa za uwekezaji na hivyo wameanza mchakato wa kuja kuwekeza na tayari kampuni moja ya Nchini Libya imeonyesha nia ya kuwekeza kwenye umeme wa maji au gesi asilia wa megawatt 400.
Hayo yamebainishwa na Balozi Arze katika mazungumzo yake na Chama cha Wafanyabishara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) alipotembelea kwenye ofisi hizo ili kuangalia fursa za kibiashara na uwekezaji baina ya Libya na Tanzania.
Katika mazungumzo hayo nchi ya Libya mbali na kuonyesha nia ya kuwekeza kwenye sekta ya umeme pia wamesema wameona kuna fursa kubwa kwenye kilimo na kwamba wanaangalia uwezekano wa kuhamasisha wawekezaji wengi zaidi kutoka Libya.
Naye Kaimu Rais wa TCCIA Octavian Mshiu amesema ujio wa balozi huyo umekuwa wa mafanikio makubwa kwani wamezungumza mambo mengi yanayoonesha nia njema katika Nyanja za biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.
“Tunashukuru kwa ujio wa Kaimu Balozi wa Libya nchini kwetu.Kikubwa ambacho Tumezungumza pamoja na mambo mengine kuna moja ya kampuni ya nchi hiyo inataka kuja nchini kuwekeza katika mradi wa umeme wa megawati 400, jambo hili limekuja wakati muafaka ambapo nchi yetu inahitaji sana uwekezaji katika Nishati ya umeme kwa ajili ya matumizi ya viwandani” Alisema Bw.Mshiu.
Aidha Bw.Mshiu ametoa rai kwa wafanyabishara nchini kuitumia TCCIA hasa kwa kuzingatia uwepo wao unalenga kuangalia fursa ambazo wafanyabiashara wanaweza kuzitumia vyema katika kujenga uchumi wa nchi.
“Mwaka huu tunatarajia kusheherekea miaka 30 ya uwepo wa TCCIA. Tumetoa mchango mkubwa katika maendeleo na dhamira yetu ni kuendelea kupanua wigo wa fursa za biashara na uwekezaji nchini, pia tunataka kuthibitisha kuwa tupo kwa ajili ya kuisaidia Serikali katika jitihada za kujenga uchumi,”Alisema.
Kwa upande wake Kaimu Balozi Arze amepongeza jitihada za TCCIA katika kuwaunganisha wafanyabiashara wa Libya na Tanzania, wanatamani kuja kuwekeza hivyo wameona ni vyema kuanza mchakato wa mazungumzo kabla ya kukutana na viongozi wa ngazi mbalimbali Serikalini.
“Kuna maeneo ambayo wafanyabiashara wetu wa Libya wanatamani kuja kuwekeza, hivyo leo nimekuja TCCIA nikiamini kuwa watakuwa sehemu ya kuwaunganisha wafanyabishara wetu. Tunataka pande zote mbili zinufaike na fursa za kibiashara zilizopo,”alisema Kaimu Balozi huyo.
Mkurugenzi wa TCCIA Fatma Hamis amesema nia kubwa la Kaimu Balozi wa Libya ni kuhakikisha sekta ya biashara inapewa kipaumbele kati ya Tanzania na Libya pia kuwaunganisha wafanyabiashara na wawekezaji wa pande zote mbili.