Hali ya sintofahamu imeibuka baina ya mikoa ya Mwanza na Geita baada ya Mkuu wa mkoa wa Geita Robert Gabriel kusitisha usafirishaji wa madini ghafi kwenda Mwanza huku Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella akisema masuala ya biashara na uchumi hayana mipaka endapo sheria na kanuni zilizopo zitatekelezwa. Mkuu wa mkoa wa Geita ameeleza kuwa amefikia maamuzi hayo ili kutoa fursa zaidi za ajira mkoani kwake na kuwezesha wananchi kufaidika na utajiri huo.
Kwa upande wake, Mongella amefafanua kuwa biashara na uchumi ni sekta ambazo hazipaswi kuwekewa mipaka, bali inatakiwa kufuata sheria na kanuni zikiwemo za malipo ya ushuru na kodi. Ameongeza kuwa ukuaji wa teknolojia umewezesha dunia kuwa kama kijiji hivyo hakuna sababu ya kuwekeana mipaka.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara na Wamiliki wa Viwanda vya Uchenjuaji wa Dhahabu mkoani Mwanza George Onyango amesema umoja huo unafanya jitihada za kuwasiliana na Mongella ili wakuu hao wawili wakae chini na kufikia muafaka ili kuvutia zaidi wawekezaji.