Kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na Halmashauri ya wilaya ya Korogwe, Serikali imefuta mashamba sita ya kampuni ya Mohamed Enterprises kutokana na kutoendelezwa kwa kipindi kirefu. Mashamba hayo yaliopo eneo la Mombo, Mabogo pamoja na Kwalukonge wilayani Korogwe yana ukubwa wa hekari 12,915.126 na kati ya mashamba 14 yanayomilikiwa na kampuni ya Mohamed Enterprises Mazinde wilayani humo.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mashamba hayo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula amesema lengo ya serikali kufanya hivyo ni kujenga nidhamu kwa waliopewa rasilimali za serikali kuzingatia masharti pamoja na taratibu ya uwekezaji.
Dk. Mabula amefafanua kuwa mara baada ya Halmashauri ya wilaya ya Korogwe kupeleka mapendekezo ya kufutwa kwa mashamba hayo, Wizara ya Ardhi ilifuatilia kuhusu madai ya kutoendelezwa kwa mashamba ya kampuni hiyo na baada ya kujiridhisha ikawasilisha maombi hayo kwa Rais na kuridhiwa.
Pamoja na hayo, Naibu Waziri huyo amempongeza Mkuu wa mkoa wa Tanga Martin Shigela kwa kusimamia maagizo mbalimbali tangu Rais Magufuli alipoanza kubatilisha mashamba ambayo hayajaendelezwa katika mkoa huo. Kwa upande wake, Shigela amewataka wananchi wa Korogwe kutovamia maeneo ya mashamba hayo hadi Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe itakapopanga matumizi bora ya ardhi hiyo.