Home BIASHARAUWEKEZAJI Rais Dkt. Mwinyi asisitiza fursa za kiuchumi na kuitangaza Zanzibar

Rais Dkt. Mwinyi asisitiza fursa za kiuchumi na kuitangaza Zanzibar

0 comment 261 views

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza Mabalozi wa Nchi za Afrika wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania kuimarisha ushirikiano na fursa za kiuchumi pamoja na kuutangaza utalii wa Zanzibar kimataifa.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Oktoba 21, 2024, alipozungumza na mabalozi waliotembelea Ikulu baada ya kumaliza ziara yao ya siku tatu ya kuitembelea Zanzibar, kuangalia fursa za uwekezaji na maeneo ya ushirikiano ambayo nchi hizo za Afrika zinaweza kufanya kazi na Zanzibar.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema wakati umefika kwa nchi za Afrika kuungana na kutumia rasilimali zilizopo kuinua uchumi na kubadilishana uzoefu ili kufikia maendeleo.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amewataka mabalozi hao kuangalia fursa za ushirikiano na uwekezaji, hususan katika sekta za utalii, usafiri wa baharini na usafirishaji, uvuvi na ufugaji wa vifaranga vya samaki, mafuta na gesi, na kilimo cha viungo ambacho Zanzibar ina utajiri mkubwa.

Akizungumzia sekta ya usafiri wa baharini na usafirishaji, amewataka mabalozi hao kuangalia fursa zilizopo kwenye sekta hiyo kwa kuziunganisha nchi za Afrika zilizo katika ukanda wa Bahari ya Hindi, kwani kwa pamoja nchi hizo zina uwezo wa kufanya biashara kubwa iwapo sekta hiyo itaimarishwa.

Akizungumzia suala la mafuta na gesi, Rais Dkt. Mwinyi amewaeleza mabalozi hao kwamba Zanzibar imebaini kuwa na kiwango kikubwa cha gesi, na tayari imeanza mchakato wa kugawa vitalu kwa ajili ya kuvuna rasilimali hiyo.

Mabalozi hao wanatoka Burundi, Comoro, Kenya, Malawi, Misri, Morocco, Sudan, Rwanda, Uganda, na Zambia.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter