Home BIASHARAUWEKEZAJI Serikali ya Tanzania yatumia Sh trilioni 1 kukuza uchumi, elimu

Serikali ya Tanzania yatumia Sh trilioni 1 kukuza uchumi, elimu

0 comment 132 views

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas amesema serikali imetoa zaidi ya Sh trilioni 1.05 kutekeleza miradi ya reli ya kisasa, mradi wa kusambaza umeme vijijini, mikopo ya elimu ya juu na kugharamia elimu bila malipo katika nusu mwaka wa mwaka wa fedha 2020/2021.

Dk Abbas alisema makusanyo kutoka sekta ya madini yameongezeka kwa asilimia 120 katika miezi sita ya mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo Sh bilioni 317.5 zilikusanywa.

Alisema hayo katika muhtasari wa kazi ambazo zimeanza na zinaendelea kutekelezwa katika miaka mitano ya rais John Magufuli.

Alisema ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaogharimu Sh trilioni 7, serikali ilitoa Sh bilioni 274.1 kuugharamia katika nusu ya mwaka wa bajeti Julai hadi Disemba mwaka jana.

Dk Abbas alisema “mradi wa reli ya kisasa umeshafika zaidi ya asilimia 90 kwa kipande cha Dar es Salaam – Moro chenye urefu wa kilomita 300 huku kipande cha Moro-Makutupora mkoani Singida chenye kilomita 422 kimefikia asilimia 55 na tayari serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha tatu cha Mwanza- Isaka chenye urefu wa kilomita 341.

Hivi karibuni nitatoa taarifa ya uzinduzi wa safari za treni katika kipande cha Dar hadi Moro na upokeaji wa vichwa vipya vya kisasa vya treni hiyo ya umeme”.

Kuhusu mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere alisema mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 30, katika nusu mwaka wa fedha, kiasi cha Sh bilioni 274.1 kimetolewa ambapo. Mradi huo utakamilika ndani ya miaka miwili ijayo na unagharimu Sh trilioni 6.5.

Akizungumzia mradi wa usambazaji umeme vijijini (REA), alisema kazi kubwa inaendelea na kuna mafanikio makubwa ambapo mpaka sasa vijiji 10,018 kati ya 12,317 vimefikiwa.

Kuhusu sekta ya elimu, alisema rais Magufuli anaendelea kutimiza ahadi zake na kwamba kwenye mikopo ya elimu ya juu Sh bilioni 105 zilitolewa kwa awamu ya kwanza ya mikopo ya wanafunzi.

 

 

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter