Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema serikali inataka kupitia upya Sheria ya Uwekezaji ya Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji Tanzania (EPZA) ili kuondoa sintofahamu zilizopo kuhusiana na tozo pamoja na kodi mbalimbali ambazo zinatozwa na Halmashauri na vilevile kutozwa tena na mamlaka husika. Kakunda amesema hayo baada ya kukagua shamba la parachichi la Africado wilayani Siha mkoani Kilimanjaro na kuongeza:
“Hivi sasa tupo katika mchakato wa maandalizi ya kupeleka bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya EPZA kwa ajili ya kufanya amendments (marekebisho) ili kuondoa hii mikanganyiko na malalamiko ya tozo na kodi zinazotozwa na Halmashauri na EPZA. Kimsingi, jambo hili linachangia sana kutoelewana kati ya Halmashauri na wewekezaji”
Kakunda amekubali kuwa kwa namna Sheria ilivyo hivi sasa, inapelekea kuwepo kwa sintofahamu kati ya wawekezaji na serikali kwenye masuala ya ulipaji kodi.
Pamoja na mambo mengine, Sheria hiyo inatoa mamlaka kwa muwekezaji kusamehewa kodi kwa hadi miaka 10.