Serikali inafanya mchakato katika kuwezesha Hatifungani ya Usalama wa Chakula ili kukuza Sekta ya Kilimo na kukuza mtaji wa kukopesha wakulima.
Pia imelenga kuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika nyanja zote za kiteknolojia, vifaa bora pamoja na kuongeza ukubwa wa maghala ya kuhifadhia nafaka ili iweze kununua na kuhifadhi chakula kwa wingi kwa usalama wa chakula nchini.
Akizungumza Agosti 8, 2024 katika kilele cha Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nane Nane jijini Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema “tumezungumza na mabenki, mabenki yameunga mkono na tunakwenda kuweka hatifungani ya usalama wa chakula ambapo tutapata fedha ambazo zitaiwezesha NFRA.”
Ameeleza kuwa katika kuhakikisha usalama wa chakula nchini Serikali imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa huduma za ugani kwa wakulima.
Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Kilimo kuratibu na kuwezesha kuundwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Maendeleo ya Ugani ili kuipunguzia Wizara majukumu na kuiwezesha kujikita katika masuala mengine yanayohusu sekta ya kilimo.
Ameongeza kuwa miongoni mwa mambo muhimu katika kukuza sekta ya kilimo ni pamoja na kuwa na ushirika imara, ambapo ameiagiza Wizara kuratibu Vyama vya Ushirika imara na kurejesha hadhi ya ushirika nchini.