Uongozi wa taasisi ya kimataifa ya kitaalamu (STL Group) inayosimamia kampuni sita zinazojihusisha na miundombinu, afya, elimu, biashara na mawasiliano umeonyesha nia ya kutaka kuwekeza visiwani Zanzibar. Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Amand iliyopo chini ya STL Group, Nadas Simhoni ameeleza hayo alipozungumza na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi ofisini kwake, visiwani humo.
Simhoni aliyekuwa na ujumbe wa watu wane amesema wana nia ya kuwekeza visiwani Zanzibar kwa kuwa wamevutiwa na mazingira ya kiuwekezaji na ni njia mojawapo ya kuunga mkono serikali katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi kwa ujumla.
Amand Group yenye wataalamu wa kutosha ambao tayari wamewekeza nchini Ghana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Togo, Ivory Coast na Tanzania wana uzoefu wa kutosha katika kusanifu mambo tofauti ikiwemo michoro ya majengo.
Kwa upande wake, Balozi Seif ameuhakikishia uongozi huo kuwa serikali ipo tayari kuwapa ushirikiano ili kutimiza azma yao. Hata hivyo, Balozi Seif ameuambia uongozi wa taasisi hiyo kuwa serikali imeweka utaratibu maalum wa kutoa zabuni inapotaka kuanzisha miradi yake ya uchumi na jamii.