Home FEDHA Fahamu faida ya kuwekeza kwenye vikundi

Fahamu faida ya kuwekeza kwenye vikundi

0 comment 85 views

Imekuwa ni jambo la kawaida hasa kwa wanawake kuunda vikundi kwa ajili ya kuwekeza sehemu ya kipato chao. Hivi sasa kuna vikundi vya aina mbalimbali katika jamii zetu, kuna vikundi maofisini, makanisani, mtaani na hata baina ya marafiki, lengo likiwa ni kuwekeza fedha ambazo zitaleta maendeleo au zitasaidia watu katika shughuli zao.

Mara nyingi kila kundi huwa na taratibu zake ambazo zinawaongoza wana kikundi lakini vikundi vyote vinaendana mambo kadhaa kwa mfano kila mwezi au wiki au siku kadhaa kila mwana kikundi hutakiwa kuchangia kiasi kadhaa cha fedha kwa mtunza hazina aliyeteuliwa, kila mwana kikundi anatakiwa kufuata sheria za kikundi kusika na iwapo ataenda kinyume na sheria hizo, hupewa adhabu mara nyingi kwa kulipa faini.

Utafiti uliofanywa na FinMark Trust’s Finscope mwaka 2009 ulionyesha kuwa kwa Afrika Mashariki, si chini ya watu milioni 37,000 wanajihusisha na vikundi visivyo rasmi katika jamii zao. Kutokana na ongezeko la vikundi hivyo idadi hiyo itakuwa imeongezeka zaidi kwani siku hizi wanaume nao wanajihusisha na vikundi hivyo.

Faida zake:

Kupata mikopo na fedha zaidi. Baada ya kukusanya fedha kwa kipindi fulani katika vikundi hivyo, wahusika na muda mwingine hata wale wasiohusika na vikundi hivyo huruhusiwa kukopa na kurudisha kwa riba ili kuzalisha zaidi fedha hizo. Kupitia vikundi hivyo watu hunufaika hasa pale wakipata shida au wakati wa mgao watu hunufaika na fedha zaidi kwa sababu vikundi hivyo huwa kama vibubu lakini vyenye faida ambazo hutokana na riba zinazotokana na mikopo.

Rahisi kuweka akiba. Kwa ambao wana matumizi mabaya, vikundi vinawapa urahisi katika kujiwekea akiba hasa kwa sababu mhusika hutakiwa kuchangia kila baada ya muda hivyo ni rahisi kuweka bajeti na akiba kwa pamoja.

Watu wengi wamenufaika na vikundi hivyo kwenye upande wa mawasiliano hasa ya kibiashara kwani kupitia mikutano katika vikundi hivyo watu wameweza kufahamiana vizuri, kujua shughuli wanazofanya na namna ya kusaidiana ili kuchochea maendeleo.

Kupitia vikundi hivyo, imekuwa rahisi kwa watu kukamilisha shughuli za kijamii ambazo huhitaji kiasi kikubwa cha fedha ambazo mara nyingi watu wanakuwa hawana. Kwa mfano ujenzi wa shule, visima n.k.

Kwa ujumla, vikundi visivyo rasmi vina manufaa makubwa kwa jamii na katika upande wa kimaendeleo kama sheria na kanuni za vikundi hivyo zinafuatwa. Ni muhimu kuwekana sawa kuhusu madhumuni na malengo ya kikundi husika na kujihusisha na vikundi ambavyo vina sheria na kanuni ambazo mwisho wa siku inakuwa ni vigumu kwa wahusika kuzivunja kwani hali hiyo husababisha matatizo kama kutolipa madeni, kukimbia na fedha au hata kutohudhuria katika mikutano.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter