Home BIASHARAUWEKEZAJI Tanzania namba moja uwekezaji Afrika Mashariki

Tanzania namba moja uwekezaji Afrika Mashariki

0 comment 121 views

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania inashika namba moja kwa uwekezaji katika nchi za Afrika Mashariki na kwamba imefanikiwa kuvutia uwekezaji wa dola za Marekani 1.18 bilioni, ikifuatiwa na Uganda (dola bilioni 0.7) na Kenya (dola bilioni 0.67). Majaliwa amesema hayo bungeni Dodoma alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mapitio na muelekeo wa kazi za serikali pamoja na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2019/2020.

“Kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali kuvutia uwekezaji nchini, hali ya uwekezaji imeimarika ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zinaonyesha kuwa Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki”. Ameeleza Majaliwa.

Katika maelezo yake, Waziri Mkuu amesema Taarifa ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) ya mwaka jana imeonyesha kiasi hicho cha uwekezaji huku ile ya “Where to Invest in Africa” nayo ikionyesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya saba kati ya nchi 52 zinazoongoza kwa uwekezaji Afrika.

“Taarifa nyingine ya “The Africa Investment Index (AII) 2018” inaonyesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 13 kati ya nchi 54 za Afrika katika kutoa fursa za masoko na vivutio vya uwekezaji”. Ameongeza Majaliwa.

Pamoja na hayo, Waziri Mkuu pia ametoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwenye ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na vilevile uwekezaji kwenye sekta ya miundombinu kwa kuwekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter