Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa pongezi kwa Kampuni ya Total Tanzania kwa kuwekeza kiasi cha shilingi bilioni 460 kwa kipindi cha miaka mitatu. Waziri huyo ametoa pongezi hizo kwenye sherehe ya kutimiza miaka 50 kwa kampuni hiyo nchini zilizofanyika Jijini Dar es Salaam.
“Tangu mwaka 2015, Kampuni ya Total imekeweza hapa nchini mtaji mkubwa wa zaidi ya dola za Marekani milioni 200 ili kutoa huduma za uagizaji, uuzaji na usambazaji wa bidhaa za mafuta ikiwemo mafuta ya dizeli, petrol, vilainishi mbalimbali na bidhaa za nishati mbadala (solar product)” amesema Majaliwa.
Mbali na hayo, Waziri huyo amesema kupitia kampuni hiyo Watanzania zaidi ya 800 wamenufaika na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutoka katika kampuni hiyo. Huku kampuni hiyo ikitoa shilingi milioni 25 kila mwaka kama mchango katika masuala ya usalama barabarani.
Pia ameipongeza kampuni hiyo kwa kuendelea kuchangia katika masuala ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuchangia katika ujenzi wa madarasa (milioni 45), ujenzi wa vituo vya afya (milioni 80), uchangiaji wa madawati katika baadhi ya shule zilizopo jijini Dar es Salaam, na uwekezaji wa zaidi ya shilingi milioni 200 kwa wajasiriamali.
“Tumeanza utekelezaji wa mpango mkakati wa kuboresha Mazingira ya Uwekezaji wa biashara nchini (blueprint) na tunafanya mapitio ya vivutio mbalimbali vya uwekezaji ikiwemo vivutio vya kikodi kupitia timu maalumu” ameeleza.