Na Mwandishi wetu
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Dk. Reginald Mengi amesema wakati wa hafla ya kumuaga Balozi wa China anayemaliza muda wake hapa nchini Dk. Lu Youqing kuwa, katika muda wa miaka sita ambao balozi huyo amekuwa hapa nchini ameunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na China, huku akiongeza kuwa uwekezaji wa nchi hiyo hapa nchini hadi kufikia Mei mwaka huu umefikia Dola za kimarekani 6.6 bilioni.
Dk. Mengi amesema China imetekeleza miradi mikubwa ya ujenzi hapa nchini ikiwemo ujenzi wa Daraja la Nyerere la Kigamboni na kusema kiwango cha biashara kati ya Tanzania na China kimeongezeka na kufikia hadi trilioni tisa kwa fedha za kitanzania, hivyo kusisitiza kuwa kwa hivi sasa, China ni rafiki mkubwa sana wa Tanzania kibiashara.
Mwenyekiti huyo pia amesema taasisi ya sekta binafsi inamuunga mkono Rais Magufuli katika jitihada za kujenga uchumi wa viwanda huku akiongeza kuwa sekta binafsi watashirikiana na serikali ili kutimiza lengo la kuimarisha sekta ya biashara hapa nchini.
Kwa upande wake, Balozi Youqing amesema atakuwa mwanachama wa TPSF kuanzia sasa na kuahidi kurejea hapa nchini ili awe mwanachama kamili na kuendelea kujishughulisha katika masuala mbalimbali ya kiuchumi.