Home BIASHARAUWEKEZAJI Watumishi washauriwa kujifunza uwekezaji mapema

Watumishi washauriwa kujifunza uwekezaji mapema

0 comments 58 views

Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi wameshauriwa kujifunza kuhusu uwekezaji mapema ili kuhakikisha kuwa baada ya kustaafu wanaendelea kuishi maisha mazuri, kama walivyokuwa kazini.

Ushauri huo umetolewa na Afisa Masoko Mwandamizi, Kampuni ya Uwekezaji ya UTT – AMIS Rahim Mwanga wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa kwa watumishi wa Halmashauri ya jiji la Mwanza na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake.

Aliongeza kuwa kustaafu hakupaswi kuwa chanzo cha matatizo ya kifedha kwa mfanyakazi yoyote aliyekuwa analipwa mshahara bali iwe fursa ya kufurahia matunda ya kazi ya muda mrefu.

“Tukijijengea utamaduni wa kuwekeza mapema kutatusaidia sisi wafanyakazi kuepuka changamoto za kifedha baada ya kustaafu na kuwa na maisha ya uhakika”, alisema Mwanga.

Aidha aliwasisitiza wafanyakazi wote nchini kuhakikisha michango yao inalipwa kwa wakati na waajiri wao lakini pia watumie Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inayotoa faida kubwa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Erick Mvati, aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kufika katika Mkoa wa Mwanza kutoa elimu ya fedha ambayo ni muhimu kwa wananchi ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Aliongeza kuwa elimu hiyo ikifika kwa wananchi wote katika makundi mbalimbali itasaida kupunguza matatizo katika jamii kwa kuwa wananchi wataelewa haki zao lakini pia watajua sheria mbalimbali zitakazowaongoza na kujiepusha na migogoro ya mikopo.

Naye Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha,  Stanley Kibakaya alisema kuwa Wizara inaendelea na zoezi la utoaji elimu ya fedha kwa wananchi ili wafahamu fursa mbalimbali zinazopatikana katika Sekta ya Fedha.

Aliongeza kuwa Sekta ya Fedha imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali, kupitia elimu hiyo inayoendelea kutolewa wataalamu hao wanapata fursa ya kusikiliza changamoto, ushauri na maoni yanayotolewa na wananchi kwa ajili ya kufanyiwa utatuzi zile ambazo zinatakiwa kufanyiwa utatuzi, ushauri na maoni kwa ajili ya kuboresha zoezi hilo kwa mikoa ambayo haijafikiwa.

Serikali kupitia Wizara ya Fedha inaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa kada zote ili kuwajengea uelewa kuhusu usimamizi bora wa fedha.

Zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha unaolenga kuimarisha ustawi wa kifedha kwa miaka 2021/2022 hadi 2029/2030.

Mpaka sasa, programu hii imefikia mikoa 16 nchini, ikiwemo Kagera, Singida, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Kigoma, Pwani, Morogoro, Rukwa, Lindi, Mtwara, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mara, na Mwanza. Wakazi wa mikoa hiyo wamepata fursa ya kujifunza mbinu za kuboresha maisha yao kupitia matumizi sahihi ya rasilimali za kifedha.

Katika utekelezaji wa mpango huu, Wizara ya Fedha inashirikiana na taasisi mbalimbali za serikali kama Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), na Bodi ya Bima ya Amana (DIB). Ushirikiano huu unalenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa maarifa kuhusu uwekezaji, akiba, na usalama wa fedha.

Aidha, benki mbalimbali nchini zimejitokeza kusaidia juhudi hizi kwa kutoa elimu kuhusu huduma za kifedha. Benki Kuu ya Tanzania (BoT), pamoja na benki za biashara kama TCB, NMB, CRDB, na NBC, zimekuwa zikishiriki katika mafunzo na semina mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wananchi kusimamia fedha zao vyema.

Kwa kupitia Elimu ya Fedha, wananchi wanapata uelewa kuhusu umuhimu wa kupanga bajeti, kujiunga na vikundi vya kifedha, na kulinda mali zao kwa kukata bima. Wizara ya Fedha inaendelea kusisitiza kuwa elimu ya fedha ni nyenzo muhimu katika kuinua uchumi wa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!