Madini ya Bati (Tin) yameendelea kuwa na mchango kwenye maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini mkoani Kagera huku watanzania wakitakiwa kuchangamkia fursa za uchimbaji wa madini hayo.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Kaimu Afisa Madini mkoa wa Kagera, Nobert Mkopi amesema, mkoani Kagera kuna fursa nyingi zikiwemo za huduma za maabara kuweza kufanyia uchunguzi wa madini yanayopatikana, makampuni ya ulinzi kwenye migodi na wafanyabiashara wakubwa wa madini, makampuni ya uuzaji mitambo pamoja na fursa za leseni za uchimbaji mdogo na mkubwa.
“Watu waje wawekeze kwenye uchimbaji wa madini ya Bati, maeneo bado yapo mengi katika maeneo ya Nyaruzumbura , Katera , Murongo.
Wilayani Kyerwa, uchimbaji unaoendelea ni mdogo wa maduara, wachimbaji wakubwa kutoka ndani na nje tunawakaribisha,” amesema Mkopi na kuongeza,
“Soko la madini ya Bati linakua, kwa sasa madini hayo yameendelea kuchangia katika maduhuli yatokanayo na Sekta ya Madini mkoani hapa,”amesema.
Amesema, madini ya bati yana matumizi mbalimbali ikiwemo kutumika kuunganisha vitu mbalimbali kama mabomba ya chuma na metali (Steel/ Metal), mifumo ya umeme (electric circuit), mifumo ya kielektroniki ya simu, vyuma vya reli, mifumo ya ndege na mifumo ya lifti za umeme kwenye ghorofa.
Pia, madini hayo hutumika kuzuia kutu kwenye vyombo vya kuhifadhia vyakula kwa muungano wa madini ya chuma. Bati vilevile hutumika kuzuia kutu kwenye mabati ya kujengea nyumba.
Aidha, Mkopi akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini hayo amewataka kufanya shughuli zao za uchimbaji kwa weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali na kupiga marufuku utoroshaji wa madini.
“Wachimbaji wa haya maeneo mmepewa leseni mchimbe kwa kufuata sheria na miongozo ya Serikali, na kinachopatikana kiingie kwenye mfumo sahihi, atakayepatikana anachepusha madini yetu kupeleka nchi nyingine bila utaratibu, atachukuliwa hatua za kisheria,” amewatahadharisha Mkopi.