Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa amesema mtambo wa kisasa uliozinduliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa ajili ya kudhibiti matumizi ya huduma za mawasiliano kwa kampuni za simu na watumiaji, utawezesha kuangalia simu zinazotoka na kuingia kwenda mitandao mingine pamoja na gharama zinazotozwa. Waziri huyo ameeleza kuwa, mtambo huo utasaidia kudhibiti malipo ya ziada na yale ya kijanja na hivyo kutatua kero ya muda mrefu ya watu kulalamika kukatwa fedha kwenye simu zao za mkononi pasipo sababu za msingi.
Prof. Mbarawa amesema hayo baada ya kukagua mtambo huo na kuongeza kuwa, teknolojia hiyo itadhibiti ulaghai unaofanywa na kampuni za simu, itaonyesha miamala ya fedha inayotumwa na pia itasaidia kukusanya mapato sahihi. Mbarawa amedai serikali imekuwa ikiwekeza kwenye sekta ya mawasiliano kwani inazidi kukua kwa kasi.
Aidha, mfumo huo wa kisasa utasaidia mamlaka husika kuona kila kitu kinachoendelea katika kampuni za simu kwa upande wa fedha .
Akizungumzia teknolojia hiyo, Mtafiti Mwandamizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka TCRA Emmanuel Manasseh, amesema mtambo huo unalenga kuhakiki mapato ya watoa huduma na kukusanya taarifa zote za waongeza salio kwa kutumia kadi za kukwangua, elektroniki, mawakala na kukusanya taarifa zote za kutumia huduma za mawasiliano.