Home BIASHARABIASHARA NDOGO NDOGO Wauza chakula barabarani wanakosea?

Wauza chakula barabarani wanakosea?

0 comment 37 views

Katika harakati za kujitafutia riziki, kila mmoja wetu anatumia ujuzi na ubunifu alionao katika namna ambayo itamuingizia kipato. Katika kufanya hivyo, wengine wanalazimika kufanya kazi katika mazingira hatarishi ambayo kimsingi humfanya mtaka huduma ajifikirie mara mbili. Sio kwamba wafanyabiashara hawa wanapenda kufanya kazi katika mazingira haya, lakini hali ngumu ya maisha inawalazimu wao kujitafutia kipato kwa namna hii.

Mfano hai wa hili ni watoa huduma ya chakula au kwa jina ambalo limezoeleka mama lishe wanaofanya kazi pembezoni mwa barabara hususani katika vituo vya mabasi. Japokuwa idadi ya wanaohitaji huduma hiyo katika maeneo kama haya ni kubwa, mazingira wanayofanyia kazi watu hawa ni haratishi. Lakini wameruhusiwa na nani? Wanazingatia usafi na afya ya wateja wao kwa ujumla? Mamlaka husika zinachukua hatua gani?

Mama lishe wengi wanafanya kazi katika maeneo ambayo kimsingi hawatakiwa kuendesha shughuli hizo. Jiulize kama wanatoa huduma ya chakula pembezoni mwa barabara, wanapata wapi maji? Je ni masafi? Wanaosha wapi vyombo vyao? Vipi kuhusu vumbi, jua kali na mvua? Bila shaka hizi ni changamoto ambazo wanazifahamu lakini bado wanaendelea kufanya shughuli zao kwa sababu wanahitaji kujiingizia kipato.

Ukiachana na mama lishe, makundi mengine ya wafanyabiashara pia wanakumbwa na changamoto hii. Pembezoni mwa barabara imekuwa sehemu yao ya kufanyia kazi bila kuangalia hatari ambazo wanaweza kukumbana nazo. Wengi wamekuwa na mitaji midogo hivyo wanashindwa kumudu gharama za pango na kuishia kufanya biashara zao katika maeneo ambayo sio rasmi ili tu waweze kujiingizia chochote.

Changamoto kwenye upatikanaji wa mikopo kwa walio na biashara ndogondogo kwa kiasi kikubwa inasukuma kuendelea kwa hali hii katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Wafanyabiashara hawa watajiboresha vipi kama taasisi husika hazitawapitia mikopo? Wataendeleza vipi biashara zao na kutoa huduma bora zaidi ikiwa hawapati msaada wowote?

Ni muhimu kama wafanyabiashara wa aina hii wakaungana kwa pamoja na kushauriana ni vipi wanaweza kukuza na kuboresha biashara zao. Waanzishe vikundi vyao wa vicoba ambavyo vitawasaidia kukopa na pia wasichoke kufanya michakato ya uombaji mikopo katika taasisi za kifedha. Ni wazi kuwa hakuna anayependa kufanya kazi katika mazingira magumu, hivyo watu hawa wakisaidiwa, wataweza kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma wanazotoa.

Japokuwa kila mmoja wetu anafanya jitihada za kupambana na umaskini, kwa biashara muhimu kama chakula, lazima mhusika ahakikishe kuwa mtaji alionao unajitosheleza na pia anazingatia mazingira ya usafi katika kazi yake ili kuepusha athari zozote zinazoweza kutokea. Aina hii ya biashara pia haina budi kufanywa katika mazingira yenye usalama ili kuwavutia wateja wengi zaidi.

 

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter