Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Zanzibar bado inahitaji wawekezaji zaidi kwani yapo maeneo mengi yenye fursa za uwekezaji ambayo hayajafikiwa na kutangazwa kimataifa.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo Septemba 17, 2024 Ikulu, Zanzibar alipokutana na timu ya wawekezaji kutoka bara la Asia.
Aidha Rais Dk. Mwinyi ameyataja maeneo yanayohitaji uwekezaji zaidi ni pamoja na utalii wa mikutano, michezo, utalii wa afya na utalii wa matamasha na kuwahimiza wawekezaji hao wajikite kwa utekelezaji wa haraka wa dhamira yao kwani Serikali ipo tayari kufanikisha azma zao.
Naye, Mratibu wa ugeni huo, Rajiv Desai ambae pia ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Utalii ya ‘Swahili Safari’ amesema kampuni yake imeandaa mkakati maalum wa kuwaunganisha wawekezaji kutoka Dubai na India kuja kuwekeza Zanzibar kutokana na kuvutiwa kwa maumbile ya kijiografia yenye ushawishi wa utaalii na ukarimu wa Wazanzibari.
Pia kulizinduliwa Jarida la “BlitzIndia” lenye nia ya kuitangaza kimataifa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla hasa kwenye nyanja za uchumi, maendeleo, utalii, sanaa na utamaduni, ambapo Rais Dk. Mwinyi alikabidhiwa nakala ya Jarida hilo lililozinduliwa rasmi Ikulu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akitazama Jarida la “BlitzIndia” Ikulu Zanzibar.