Home BIASHARA ZIFAHAMU MBINU ZA KUKUZA BIASHARA YA CHAKULA

ZIFAHAMU MBINU ZA KUKUZA BIASHARA YA CHAKULA

0 comment 714 views

Sote lazima tule ili tufanikishe majukumu yetu ya kila siku. Hii ni sababu mojawapo ya biashara ya migahawa kuwa maarufu zaidi hapa nchini kama ilivyo sehemu mbalimbali duniani kote. Chakula ni hitaji la kila binadamu ndio maana aina hii ya biashara imefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Sio kweli kuwa muda wote migahawa inaingiza faida na kudumu kwani tumeona biashara kama hizi zikipata hasara na kufunga. Kabla ya kuingia katika biashara ya chakula ni muhimu kuzingatia haya yafuatayo.

Ni lazima kuanzisha biashara hii katika eneo ambalo lina wateja wengi. Bila kuwa na wateja biashara hii kama zilivyo biashara nyingine haiwezi kuzaa matunda. Ni lazima iwepo katika eneo ambalo wateja wanaweza kulifikia kwa urahisi asubuhi, mchana na usiku. Biashara hii lazima iwepo mahali ambapo watu wataiona kama barabarani ama eneo ambalo halikosi watu wengi kama hospitali, vituo vya magari, eneo la masoko n.k.

Ili kuhakikisha kuwa mgahawa wako unakuletea faida pia ni muhimu kuzingatia usafi wakati wote. Hakuna mtu ambaye atataka kula sehemu ambayo siyo safi kwani hali hiyo inahatarisha afya yake. Kama unafikiria kuanzisha biashara hii hakikisha eneo lako la kazi kuanzia jikoni mpaka wanapokaa wateja wako ni safi. Sio hivyo tu, hakikisha vyakula vinawekwa katika mazingira masafi, vyombo ni visafi na huoshwa pale vinapotumika. Ni muhimu pia kuanisha biashara hii ukiwa na uhakika wa huduma ya maji muda wote.

Jambo la tatu la kuzingatia kabla ya kufungua biashara ya chakula ni ubora wa chakula chako. Sio jambo la kushangaza kuwa biashara hii ipo kila mahali lakini ni muhimu kujiuliza kwanini wateja hawa waje kufuata huduma hii kwako? Kuwa makini katika kuamua ni aina gani ya chakula unategemea kuuza na pia hakikisha vyakula vyote vina ubora, vina ladha, ni vitamu, hakikisha unazingatia lishe bora na pia ikiwezekana, ni vizuri kwa mmiliki wa biashara hii kusimamia maandalizi yote ya chakula ili kujiridhisha nayo kabla ya kuvitarayisha kwa wateja wake. Pia ni muhimu kuweka bei ambayo ni rafiki na wateja wanaweza kumudu. Bei inapaswa kuendana na huduma hivyo ni vizuri kuhakikisha kuwa chakula chako ni bora na bei inaendana na kiwango chake.

Kabla ya kufungua biashara ya chakula kuwa idadi ya wahudumu inajitosheleza. Ili biashara kama hii iende vizuri ni jambo la muhimu kuwahudumia wateja kwa haraka bila kuwachelewesha hivyo uwepo wa wahudumu wengi ambao wataweza kuhudumia wateja wote wanaofika hapo kwa haraka inachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya biashara hii. Wakati unaanza unaweza kuwa na wahudumu wachache lakini biashara inavyozidi kukua idadi ya watoa huduma nayo lazima ikue.

Jambo la mwisho katika biashara ya migahawa ni kuhakikisha kuwa unakuwa mbunifu. Kazi yoyote inayofanywa bila ubunifu ni sawa na kazi bure. Wape wateja wako kitu tofauti. Hakikisha huduma zako ni tofauti na mgahawa uliopo mtaa wa nyuma yako. Ubunifu katika sekta yoyote ile unavutia wateja hivyo usisahau kufanya hivyo katika biashara hii na bila shaka utafanikiwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter