Lengo la sheria katika kila jamii ni kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda sawa na kila mtu anafanya shughuli zake bila changamoto yoyote kutoka aidha kwa wananchi wenzie au serikali. Katika biashara pia, wafanyabiashara wamewekewa sheria za kufuata ili kurahisisha shughuli zao.
Zifuatazo ni baadhi ya sheria ambazo mfanyabiashara anapaswa kuzifuata:
Sheria ya Makampuni ya mwaka 2002
Mwenye kampuni au biashara aliyesajili biashara yake hutakiwa kufuata kanuni zinazohusu Sheria hii. Ikiwa mhusika atapuuza matakwa yaliyopo katika sheria hii, basi hupewa faini au hata kufikishwa mahakamani. Ni muhimu kila mfanyabiashara kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Vipengele vya sheria hii:
- Kuwasilisha mapato ya kila mwaka yanayohusu maelezo yote muhimu ya kampuni husika, ikiwa ni pamoja na maelezo juu ya hisa, uongozi, amana na gharama nyinginezo
- Kuwasilisha mahesabu yaliyokaguliwa.
- Kuwasilisha mabadiliko yoyote ya taarifa za kampuni kama vile jina la kampuni, malengo na madhumuni ya kampuni, Bodi ya wakurugenzi, mtaji wa kampuni, madaraja ya hisa, anwani ya ofisi iliyosajiliwa, uteuzi wa wapokeaji, mameneja, maafisa utawala pamoja na taratibu za kufunga biashara au kampuni husika.
- Malipo ya kodi mbalimbali za serikali kuu na serikali za mitaa.
Sheria ya Leseni
Kufanya biashara bila leseni ni kosa la jinai kwa mfanyabiashara yeyote nchini. Sheria hii imeweka wazi katika sura ya 208 kuwa hairuhusiwi kufanya biashara bila leseni ya biashara.
Kila leseni ya biashara inatolewa kwa ajili ya biashara husika na katika eneo husika, labda kama kuna eneo maalumu la biashara ambapo leseni ya biashara husika zinatolewa au kama hakuna ada ya biashara inayoelezwa kulingana na biashara husika.
Mamlaka za leseni zina uwezo wa kufunga maeneo ya biashara yanayoendeshwa bila leseni. Kwa kufanya hivyo, mamlaka inaweza kuomba msaada wa polisi au mamlaka nyingine iliyoidhinishwa. Ili kuondokana na changamoto kama hiyo, mfanyabiashara hushauriwa kupata leseni ya biashara kabla hajaianzisha rasmi.
Sheria ya Hakimiliki
Sheria hii inafanya kazi zaidi katika masuala ya uvumbuzi wa teknolojia, huduma na bidhaa. Mtu yoyote anayezindua bidhaa au teknolojia fulani ana haki ya kutoa malalamiko iwapo bidhaa aliyoanzisha imetumika kinyume na sheria.
Pia kupitia sheria hii watu wengine huruhusiwa kutumia bidhaa, huduma au teknolojia fulani ili mradi wafuate masharti elekezi.
Sheria ya Bima
Wafanyabisahara wengi hawatilii maanani kipengele cha bima hadi pale majanga yatakapotokea. Ifahamike kuwa bima ni muhimu kwa mfanyabiashara yeyote kwa sababu hakuna anayejua kitakachotokea mbeleni.
Kuna aina nyingi za bima kwenye biashara zikiwemo bima ya moto, bima ya wizi, bima ya gari, hata bima ya afya ni muhimu kwenye biashara. Sheria hii imelenga kumuongoza mfanyabiashara na watoaji wa huduma za bima.
Sheria ya Mikataba
Kila kampuni au biashara huwa na mikataba mbalimbali, sheria hii imewekwa kwa lengo la kuhakikisha mikataba hiyo inafuatwa baina ya kampunina muhusika aliyefanya mkataba huo. Iwapo kampuni haitokamilisha makubaliano ya mkataba husika basi sheria hii huingilia kati ili kuhakikisha haki inafanyika katika pande hizo mbili.
Kwa ujumla, sheria ni nyingi, mfanyabiashara anachotakiwa kufanya ni kuzingatia sheria hizo kama anataka biashara yake ikue, urahisi wa kupata mikopo, kujenga mahusiano mazuri na kampuni au wafanyabiashara wengine.
Ni muhimu kwa mfanyabisahara kuwasiliana na wataalamu kabla hajapiga hatua yeyote ili kuepukana na kuvunja Sheria kwa ujumla.