Home Elimu BoT yazindua mtaala wa Wakufunzi Elimu ya Fedha

BoT yazindua mtaala wa Wakufunzi Elimu ya Fedha

0 comment 180 views

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba amezindua Mtaala wa Wakufunzi wa Elimu ya Fedha waliorasimishwa katika Ofisi za Makao Makuu Ndogo ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

Akizindua mtaala huo, Gavana Tutuba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Huduma Jumuisha za Fedha amesema utekelezaji wa mtaala huu utasaidia kutatua changamoto zinazotokana na uhaba au upungufu wa ujuzi wa usimamizi binafsi wa masuala ya fedha.

“Changamoto hizi zinaweza kusababisha uzorotaji wa ufanisi wa wafanyakazi katika taasisi za fedha tunazosimamia na kuathiri mfumo wa fedha nchini au kusababisha ongezeko la mikopo chechefu kutokana na wakopaji kutokua na umakini na ujuzi binafsi wa kusimamia masuala ya fedha,” amesema.

Ameongeza kuwa Baraza la Huduma Jumuishi za Fedha linaazimia kwamba changamoto hizo zitamalizwa huku akisisitiza utekelezaji wa mtaala huu utatimiza azma hiyo.

Pamoja na kutoa pongezi kutokana na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika utunzi wa mtaala huu Gavana Tutuba ameiagiza Sekretarieti ya Baraza la Huduma Jumuishi za Fedha kuhakikisha kuwa utekelezaji wa programu hii unakuwa endelevu, shirikishi, wenye ubunifu, uweze kupimwa na utolewe taarifa.

Awali, Naibu Gavana Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Sauda Msemo, alisema mtaala huo una lengo la kukuza maadili katika matumizi ya fedha.

Ameeleza kuwa uzinduzi wa mtaala huu ni kielezo cha jitihada zinazoendelea kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya fedha kutokana na umuhimu wake katika ustawi wa uchumi wa nchi.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, Beng’i Isaa amesema kutokua na elimu ya masuala ya fedha kunapelekea wananchi hususani wanawake kufanya maamuzi yasiyo na tija ikiwemo kuchukua mikopo ‘kausha damu’ bila kujua hasara zake.

Kwa upande wake Prof. Andrew Mbwambo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Iringa, ambacho ni miongoni mwa vyuo vyilivyoingia makubaliano na BoT katika kutoa elimu hiyo, ameipongeza Benki Kuu kwa kushirikisha vyuo vya serikali na vyuo binafsi katika maandalizi ya mtaala huo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter